Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bi. Wamoja Ayubu (Kushoto) akipokea moja ya Ipad toka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel kwa msaada wa kampuni ya Star Times kwa ajili ya Maafisa Habari wa Mkoa na Halmashauri za Mkoa wa Iringa.
Uwanja wa Kisasa uliojengwa na Kituo cha Michezo cha Iringa Footbal For Hope kwa ufadhili wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa ajili ya kukuza vipaji vya watoto na kuwafikishia vijana kwa kuwapa elimu ya Afya kupitia michezo.
Baadhi ya Wadau wa Sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Ole Gabriel (hayupo pichani) wakati alipokutana nao jana mkoani Iringa.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyechuchumaa chini) akipewa maelezo kuhusu kazi za Sanaa zilizowekwa katika Makumbusho ya Boma la Wajerumani lililopo mkoani Iringa jana, kulia kwake ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Bwana. Jimson Sanga ambaye ni mmoja wa Waratibu wa Makumbusho ya Boma hilo.
Na Zawadi Msalla- Iringa.
Wanahabari wa Mkoa wa Iringa wameeleza masikitiko yao ya ukosefu wa Mikataba ya ajira ambayo inasababisha upotevu wa haki zao za msingi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.Wakieleza masikitiko hayo mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel jana alipotembelea mkoa huo kujionea shughuli mbalimbali za kisekta za Wizara hiyo walisema ni kwakipindi kirefu sasa tatizo hiloni kilio chao.
Wadau hao wa habari walidai kukosekana kwa mikataba ya kazi imekuwa ni kikwazo kikubwa kinacho wakatisha tamaa na hivyo kuitaka Wizara iangalie kwa umakini suala hilo na kuliingiza katika sheria tarajiwa ya habari.
Akiwakilisha maoni yake Bwana Leonard Frank alisema waandishi wengi wanategemea bahasha katika kuendesha maisha yao ya kila siku kwakuwa hawana mikataba ya ajira hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maisha ya wana habari kuwa duni.“Hakuna mishahara,Malipo stahili sawasawa na kazi zetu wala maslahi nyingine zozote”alisema.
Aidha waliiomba Serikali kuangalia namna ya kukaa na wamiliki wa vyombo vya habari ili kuweza kujadili suala hilo na kutafutia ufumbuzi wa kudumu.Naye Katibu Mkuu akijibu hoja hiyo aliwataka wamiliki wa vyombo vya Habari wasisubiri mpaka sheria mpya ya habari itoke iliwaweze kutatua suala hilo kwani ni haki ya msingi ya mtu yeyote anaye fanya kazi.
Alisisitiza kuwa kulipa vizuri waandishi wa habari itasaidia waandishi kufanya kazi kwa moyo na kukuza vyombo vyao.“Sheria isishurutishe watu, haki ya msingi ya kibinadamu lazima ibaki kuwa haki ya msingi kama kweli wamiliki mnahitaji matokeo mazuri zingatieni suala zima la mikataba”Alisema Profesa Gabriel.
Pia aliwataka waandishi wa habari wajiweke vizuri ili thamani yao ionekane na kuongeza kuwa imefika wakati wa waandishi kuhakikisha jamii inatambua kuwa bila uwepo wao mambo hayawezi kwenda vizuri.“Hakuna atakaye kuthamini kama hauoneshi kwanini una umuhimu wa kuwepo hapo, kama mwajiri wako haoni tofauti ya uwepo wako au kutokuwepo kwako basi haina haja ya kulilia mkataba” Aliongeza Profesa Gabriel.Aliwaambia Wizara yake ipo katika mkakati wa kuinua sekta zake nne ili ziweze kutambulika na kuonekana katikati ya jamii.