Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha na Meneja Mwandamizi wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Issa Hamisi (katikati) akizungumza juu ya utendaji wa benki yake katika robo ya pili ya mwaka 2014 jijini Dar es Salaam jana. Pamoja naye ni Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu wa Benki hiyo George Binde (kushoto) na Meneja Utafiti na Uchambuzi Biashara Bw. Joseph Mrawa.
FAIDA ya kabla ya kodi ya robo ya pili mwaka 2014 ya Benki ya Exim imeongezeka kwa asilimia 80 mpaka shilingi bilioni 9.6 kutoka kipindi kama hicho mwaka jana. “Tunayofuraha kuripoti matokeo mazuri ya robo ya pili ya mwaka,” alisema Bw. Issa Hamisi, Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim jijini Dar es Salaam jana.
“Ukuaji huu wa mapato unaashiria mafanikio yatokanayo na vyanzo vya benki tofauti vya mapato. Tunaendelea kuboresha ufanisi katika uendeshaji ili kuweza kufikia matakwa ya wateja wetu. Benki yetu ipo katika muelekeo nzuri. Tupo katika hatua nzuri ya kufikia malengo yetu. Matokeo yetu ya robo ya mbili yanaonyesha kuwa tumeendelea kufanya vizuri mwaka huu,” alisema.
Faida ghafi ya riba, limekuwa kwa asilimia 36 katika kipindi sawa na hicho mwaka 2013 mpaka shilingi bilioni 14.3. Biashara ya fedha za kigeni imekuwa katika robo hii ambapo asilimia 33 imeongezeka kwenye robo ya pili ikilinganishwa na mwaka jana. Gawio lililopokelewa katika robo ya pili toka katika vyanzo vyetu vya uwekezaji kwa Benki ya NMB na tawi letu la Comoro kwa mwaka 2013 limeonyesha kuwa chanya katika matokeo yetu mazuri.
Pato la tozo na kamisheni limeongezeka kwa asilimia 19 toka katika robo ya mwaka uliopita, hadi shilingi bilioni 6.2, lililotokana na kukua kwa biashara ya fedha za kigeni na bidhaa za kifedha za biashara baada ya utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitatu. Pato toka katika vyanzo vya uwekezaji limekuwa kwa asilimia 184 ikilinganishwa na kipindi hicho mwaka jana, hadi shilingi bilioni 4, litokanalo na ongezeko la pato la gawio lililopokelewa.
“Gharama za jumla za uendeshaji zilidhibitiwa na kukua kwa asilimia 21 tu mpaka shilingi bilioni 16.7 kutokana na gharama za uanzishwaji wa matawi mapya na motisha za wafanyakazi katika jitihada za kuongeza upatikanaji wa huduma za Benki kijeografia na kuiimarisha Benki kwa ujumla. Kwa matokeo hayo, gharama za uwiano wa pato (cost to income ratio) zimeweza kushuka toka asilimia 64 iliyopatikana katika robo ya mwaka uliopita mpaka asilimia 57,” aliongeza.
Amana za wateja zimeripotiwa kuwa shilingi bilioni 776 ikilinganishwa na robo ya mwaka uliopita zikiwa na ongezeko la amana zitokanazo na CASA (Current & Savings Accounts) katika robo hiyo la shilingi bilioni 36 ikilinganishwa na matokeo ya robo ya kwanza ya mwaka 2014. Mikopo iliyotolewa imerekodi ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na robo kama hiyo mwaka jana mpaka shilingi bilioni 558 na vivyo hivyo mizania ya benki imekua kwa asilimia 9 mpaka shilingi tilioni 1.15.
“Kipaumbele kikubwa bado kipo katika jitihada zetu za kuimarisha nafasi yetu katika soko na kuboresha utosherezaji wa mahitaji ya mteja kupitia ufanisi wa kiuendeshaji. Mwenendo thabiti katika kufikia matakwa ya mteja ni ishara tosha ya kwamba tunaweza kufanikisha malengo yetu kwa mwaka huu, "alisema kaimu Afisa Mkuu wa Fedha na Meneja Mwandamizi wa Fedha wa Benki hiyo.
Katika jitihada za kuimarisha nafasi yake ya kiushindani benki imejikita katika muundo wa kibunifu wa biashara ndogo (innovative retail model) ambao umeboresha mawasiliano na wateja na uendeshaji wa karibu zaidi wa matawi yote. Muundo huo mpya wa menejimenti katika matawi umeanzishwa mwaka 2014.
“Katika hatua ya kuboresha uendeshaji kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wateja, baadhi ya shughuli zetu kama vile za ufunguaji wa akaunti na nyinginezo vimewekwa katika mfumo mmoja. Uanzishwaji wa ‘mfumo wa uendeshaji mmoja’ umelenga katika uboreshaji wa huduma za benki pamoja na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa benki kwa ujumla,” alisema Bw. Issa Hamisi.
Benki pia imeendelea na jitihada zake dhidi ya shughuli mbali mbali za kijamii katika robo hiyo kwa kushiriki katika matukio ya kijamii na kutoa misaada. Hii ni pamoja na kuchangia magodoro katika hospitali ya Mwananyamala, kompyuta katika shule ya msingi ya Kilakala na kutoa malazi kwa wazee kupitia taasisi ya Tushikamane Pamoja Foundation (TPF).
Kutokana na utendaji huo nzuri wa robo ya pili na fursa zilizopo kwenye uchumi, Benki inategemea utendaji mzuri zaidi katika robo zifuatazo, kampeni za mauzo zikitiliwa mkazo na kuimarisha ufanisi wa kiuendeshaji.