Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan akisoma hotuba wakati wa
kufungua mafunzo kwa Wakuu wa Idara na vitengo kutoka Mkoa wa Dodoma na
Singida ya Mpango kazi wa Haki za Binadamu.
Washiriki wa mafunzo kutoka Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya
Pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan.
Washiriki wa mafunzo kutoka Mkoa wa Dodoma wakiwa katika picha ya
Pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan (katikati)akiwa katika
picha ya pamoja na Mratibu wa Mpango kazi wa Haki za Binadamu Bw. Laurenti
Buliro (mwenye suti nyeusi)na mtumishi kutoka Tume ya Haki za Binadamu na ASA
Utawala bora Bw Vicent Mbombo (kulia).
"Suala la uwajibikaji kwa watumishi wa umma wakiwemo wa Halmashauri ni
changamoto kubwa kutokana na baadhi yao kutozingatia maadili ya kazi zao,
kuendekeza rushwa, kutoa huduma zisizokidhi matarajio ya wananchi na hivyo
kusababisha malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali".
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan ameyasema hayo leo asubuhi
katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati akifungua mafunzo ya Mpango
kazi wa Kitaifa wa haki za Binadamu kwa wakuu wa idara na vitengo 60
kutoka Mikoa ya Dodoma na Singida.
Liana amesema ipo haja kubwa ya kueneneza elimu ya haki za binadamu na
misingi ya utawala bora katika jamii ili haki hizo ambazo zimeaninishwa
katika Katiba ya nchi, sheria na mikataba ya haki za binadamu itambuliwe
na kuheshimiwa na watu wote.
Ameongeza kuwa hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa za
uvunjifu wa haki za binadamu hali inayoonesha kuwa bado kuna uelewa mdogo
wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika jamii.
Liana amesisitiza kwa kutoa mifano ya taarifa za ukatili dhidi ya watoto,
matukio mbalimbali ya wananchi kujichukulia sheria mikononi dhidi ya
watuhumiwa wa uhalifu, ukatili dhidi ya wanawake na utumikishwaji wa
watoto kuwa yamekuwa yakijitokeza kwa wingi.
Tume ya haki za Binadamu inatoa mafunzo ya siku nne kwa wakuu wa Idara na
Vitengo 60 kutoka Mikoa ya Dodoma na Singida juu ya Mpango kazi wa Kitaifa
wa Haki za binadamu.
Mafunzo hayo yatajikita katika kutambua makundi mbalimbali ya haki za
binadamu ambayo ni haki ya kiraia na kisiasa, haki za kiuchumi, kijamii na
kiutamaduni, haki za makundi na misingi ya utwala bora.