Ujenzi wa mradi wa maji wa Chipingo-Mkaliwata, wilayani Masasi katika mkoa wa Mtwara ukiendelea.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akitoa msisitizo kwa Jumanne Mackenzie, mkandarasi kutoka Kampuni ya Singilimo Enterprises Ltd akamilishe mradi wa maji wa Makong’onda, uliopo katika Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Mkurugenzi Mtendaji wa MANAWASA, Mhandisi Nuntufye David akiwa na Waziri wa Maji, Makame Mbarawa kwenye chanzo cha maji cha Mbwinji.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akitoka kukagua chanzo cha maji cha Kisimani Newala kilichopo katika Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akikagua maendeProfesaleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Chipingo-Mkaliwata, wilayani Masasi katika mkoa wa Mtwara
………………………
Serikali imewekeza takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 45 kwenye miradi ya maji mkoani Mtwara kwa lengo la kufikisha huduma ya maji mkoani humo kwa asilimia 100.
Akizungumza akiwa ziarani katika Wilaya ya Masasi, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inataka ifikapo mwaka 2020 upatikanaji wa huduma ya maji nchini uwe kwa kiwango cha asilimia 95 mijini, asilimia 90 kwenye miji mikuu ya wilaya na asilimia 85 vijijini.
Profesa Mbarawa amesema ili kufikia lengo hilo mpaka sasa Serikali imetenga Shilingi Bilioni 45 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji 37 kwenye mkoa wa Mtwara pekee, ambapo mpaka sasa imeshalipa kiasi cha Shilingi Bilioni 25 na Shilingi Bilioni 20 iliyobaki italipwa kwa kadiri hati za malipo zitakapokuwa zinafika wizarani.
Amezungumza hayo mara baada ya kukagua miradi ya maji ya Makong’onda, Chipingo-Mkaliwata na kutembelea chanzo cha maji kinachotumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA).
Profesa Mbarawa amesema kwa sasa mkoa wa Mtawara una jumla ya miradi 37 inayotekelezwa na 4 kati ya hiyo imekamilika, mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji na kuahidi itakamilika kwa wakati ili kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji kwa wakazi wa mkoa huo.
Amesisitiza kuwa maeneo mengi Mtwara kuna vyanzo vya maji vya kutosha, ukiacha Wilaya ya Nanyumbu ambapo upatikanaji wa vyanzo vya uhakika ni chanamoto. Kikubwa kinachotakiwa ni usimamizi mzuri wa wakandarasi waliopewa kazi na wahandisi wanaosimia ujenzi wa miradi hiyo na kutunza vyanzo vya maji vilivyopo viweze kuwa endelevu.
Vilevile, Profesa Mbarawa amesema suluhisho la tatizo la maji katika Wilaya ya Nanyumbu ni ujenzi wa mabwawa, na hivi karibuni wataanza ujenzi wa mabwawa matatu kama mpango wa muda mfupi, wakati mpango wa muda mrefu ni kutumia mradi wa Makonde kwa kujenga matenki ya maji kwa ajili ya kusambaza maji katika wilaya hiyo.
Aidha, amekuwa Waziri wa Maji wa kwanza kufika Kijiji cha Mkwaya na kuwatoa hofu ya upatikanaji wa maji baada ya kumtaka mkandarasi kutoka Kampuni ya Singilimo Enterprises Ltd awe amekamilisha mradi wa Makong’onda ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, vinginevyo atamfukuza endapo atashindwa kuukamilisha.
Wakazi wa Kijiji cha Mkwaya kilichopo Kata ya Makong’onda wamesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta faraja kubwa kwa kuwa huduma ya maji inapatikana, ila kiwango chake bado hakitoshelezi mahitaji.