Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Gulam Remtullah, (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mda mfupi baada ya kupokea abiria wa kwanza kutumia ndege ya Shirika la ndege la Taifa Air Tanzania, baada ya shirika hilo kurejesha huduma zake mkoani Tabora, iliyositishwa kwa kipindi ya zaidi ya mwaka mmoja kupisha marekebisho ya uwanja huo. ATCL imekuwa ndege ya kwanza kubwa kuanza safari zake mkoani hapo. Kulia ni Afisa Mwongozaji wa ndege wa shirika la ndege la ATCL, Kabel Msumeno.
Abiria wa kwanza kutumia ndege ya Shirika la ndege la Taifa ya Air Tanzania, wakishuka katika uwanja wa ndege wa Tabora, baada ya kufurahia safari yao kutoka Dar es Salaam. Ddege ya ATCL imekuwa ya kwanza kubwa kuruka mkoani hapo, baada ya huduma ya safari za ndege ya abiria kusitishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja ili kupisha ujenzi wa uwanja huo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Gulam Remtullah, akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Shirika la ndege la Taifa ya Air Tanzania mda mfupi baada ya ndege ya shirika hilo kurejesha huduma zake mkoani Tabora, iliyositishwa kwa kipindi ya zaidi ya mwaka mmoja kupisha marekebisho ya uwanja huo. ATCL imekuwa ndege ya kwanza kubwa kuanza safari zake mkoani hapo.
======== ======= ========= ========
Air Tanzania yatua Tabora
NDEGE ya Shirika la Ndege la Taifa la Air Tanzania Jumamosi ilitua katika uwanja wa ndege uliokarabatiwa wa Tabora, na kulifanya kuwa ndege ya kwanza kubwa kuruka katika njia hiyo baada ya kuhairisha huduma hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja kupisha ukarabati wa uwanja huo.
Safari hiyo ilipokelewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Bw. Gulam Remtullah, ambaye alisema kuwa kuahirishwa kwa huduma za ndege kwa mwaka mmoja kumesababisha kuzorota kwa biashara mjini Tabora na mkoa wote kwa ujumla kwa kuwa mkoa huo ulibaki na barabara pekee kama kiungo muhimu na mikoa mingine, hivyo kuwa changamoto kwa maendeleo ya biashara.
“Kurejeshwa kwa safari za Ndege za Air Tanzania kumeupa mkoa nguvu mpya ya kujikita katika maendeleo zaidi. Kuna biashara nyingi zilizodhurika pamoja na huduma zinazohitaji usafiri wa haraka hazikuwa zikitolewa kwa kuwa mkoa haukuwa na shirika lolote la ndege linalotoa huduma katika mkoa wetu.
“Sasa kwa kuwa shirika letu la Ndege la Taifa limeanza kutoa huduma mkoani hapa tena, ningependa kuuomba uongozi wa shirika kufikiria kuruka Tabora kila siku kwa kuwa watu wengi wanahitaji huduma hii. Hii inathibitishwa na idadi kubwa ya abiria waliokata tiketi kwa ajili ya safari hii ya kwanza kuja Tabora na kutoka Tabora kuelekea sehemu nyinginezo. Kama shirika litaendelea kutupatia huduma nzuri, litaendelea kuaminiwa na wateja wengi zaidi,” alisema Remtullah.
Safari zilizotambulishwa zitakuwa katika siku za Jumatatu, Alhamis na Jumamosi ambapo muda wa kuruka kwa Jumatatu na Jumamosi utakuwa ni saa 5:30 asubuhi, ndege ikiruka moja kwa moja kuelekea Tabora na Jumatano saa 12:30 asubuhi ikiruka kupitia Kigoma, kwa kutumia ndege aina ya De-Havilland Dash8 – Q300 ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 50.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Kapteni Milton Lazaro, wakati wa kutangaza kuanzishwa safari za Tabora ilisema kuwa shirika hilo limejipanga kutoa huduma ya usafiri, yenye bei nafuu, salama na ya uhakika kwa abiria watakao tumia njia hiyo.
Alisema kuwa maamuzi ya uongozi wa ATCL kurejesha njia ya Tabora ni suala jema katika kutimiza azma yake ya kukuza ushirikiano wa Tabora na mikoa mingine.
“Tunaamini kurejeshwa kwa safari katika njia hii kutakuwa ni chachu ya maendeleo ya uchumi katika mkoa wa Tabora na Kanda ya Ziwa kwa ujumla,” alisema.
Kpt. aliongeza kuwa kurejea kwa njia hiyo ya Tabora kumetokana na kilio cha wananchi, maombi toka kwa mawakala wa usafiri na Bunge wakilitaka shirika la ndege la taifa kutimiza dhamira yake ya kufanya biashara na kuwahudumia wananchi.
Aidha, alibainisha kuwa shirika lake limejidhatiti kwa kuwa na mpango madhubuti ambao utapelekea shirika kufungua njia mpya nchini ikiwa ni pamoja na Songwe, na kurejesha safari za Arusha, Zanzibar na Mwanza.
“Njia hizi mpya zitaanza kufanyakazi baada ya kupokea ndege yetu mpya baadae mwaka huu. Baada ya upatikanaji wa ndege hiyo ukithibitishwa wananchi watapatiwa taarifa,” alisema.