Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, (wa kwanza kushoto), akiongozwa na Meneja Mwandamizi Miradi ya Umeme wa TANESCO, Gregory Chegere kukagua maendeleo ya mradi wa kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme katika Jiji la Dar es Salaam katika kituo cha Mbagala. Kulia ni Mhandisi wa miradi (TANESCO), Frank Mashalo. Wengine nyuma ni Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Paul Masanja (nyuma kulia) na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia maendeleo ya Nishati, James Andilile.
Meneja Mwandamizi Miradi ya Umeme wa TANESCO, Gregory Chegere (kushoto) akimweleza jambo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kulia) kuhusu maendeleo ya kituo cha usafirishaji na usambazaji umeme cha Mbagala jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kimejengwa kupitia mradi wa Tanzania Energy Development and Acess Program (TEDAP) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia. Wengine wanafuatilia ni Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Paul Masanja (nyuma kulia) na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia maendeleo ya Nishati, James Andilile, wengine ni Maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO.
Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Paul Masanja (wa pili kulia) akibadilishana jambo na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, James Andilile (wa kwanza kulia) huku Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) akibadilishana jambo Meneja Mwandamizi Miradi ya Umeme wa TANESCO, Gregory Chegere (wa pili kulia) wakati Dkt. Kalemani alipotembelea maendeleo ya ujenzi huo unajengwa na Kampuni ya SAE Power Line ya Italia kwa ushirikiano na Transrail Structures.
Mkandarasi Kampuni ya SAE Power Line ya Italia inayoshirikiana na kampuni Transrail Structures, inayojenga miradi ya kuboresha miuundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme katika jiji la Dar es Salaam kupitia mradi wa Tanzania Energy Development and Access Program (TEDAP), akimweleza jambo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) kuhusu ujenzi wa Kituo cha Kurasini wengine wanaofuatilia ni viongozi waandamizi Wizara ya Nishati na Madini, Maofisa kutoka TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza na Meneja Mawasiliano Ofisi ya TANESCO, Kinondoni Kusini. Naibu Waziri alifika ofisini hapo katika ziara ya kushtukiza ili kujua kero mbalimbali zinazokutana nazo wananchi ikiwa pia kuangalia namna ofisi hizo zinavyowahudumia wananchi. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, James Andilile. Kushoto ni Meneja wa TANESCO, Kinondoni Kusini, Gasper Msigwa.
Meneja wa TANESCO, Kinondoni Kusini, Gasper Msigwa, kulia akimweleza jambo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) wakati Dkt. Kalemani alipofanya ziara ya kushtukiza ofisini hapo kuona namna TANESCO inavyowahudumia wananchi. Nyuma ya Dkt. Kalemani na Naibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja. Kulia nyuma ni Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, James Andilile na wengine ni Maofisa wa Wizara na Wanahabari.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kulia) akiongea jambo na watumishi wa ofisi ya Huduma kwa Wateja (TANESCO) wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi ya TANESCO Kinondoni Kusini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja, wakimsikiliza Mzee Rashid Bago Mkazi wa Manzese aliyefika ofisi za TANESCO Kinondoni Kusini kupata huduma. Naibu Waziri alifanya ziara ya kushtukiza ofisini hapo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza na baadhi ya wateja waliokuwa wakisubiri kuhudumiwa sehemu ya huduma za wateja katika Ofisi ya TANESCO Kionondoni Kusini. Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja. Wengine ni Maofisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO.
Kuchelewa kwa Miradi ya umeme, DSM
ØDkt. Kalemani aagiza iendelee kutekelezwa Jan 20
Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Kufuatia kuchelewa kukamilika kwa miradi ya ujenzi wa Kuboresha miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza umeme katika jiji la Dar es Salaam kupitia mradi wa Tanzania Energy Development and Access Program (TEDAP) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, Mkandarasi Kampuni ya SAE Power Line ya Italia kwa ushirikiano na Transrail Structures, wametakiwa kukamilisha miradi hiyo ifikapo mwezi Februari mwakani.
Hatua hiyo inafuatia ziara ya Dkt. Kalemani kutembelea ujenzi wa miundombinu hiyo jijini Dar es Salaam, katika vituo vya Kurasini, Mbagala, Kipawa na Gongolamboto, inayosimamiwa na TANESCO, ambayo kukamilikwa kwake kutawezesha zaidi ya wakazi 10,000 wa jijini Dar es Salaam, kuunganishwa na nishati ya umeme.
Dkt. Kalemani ameiagiza TANESCO, kuhakikisha kuwa, hadi ifikapo tarehe 15 Januari mwakani, iwe imekwishawalipa fidia wakazi 83 wa Mbagala Charambe, Kiburugwa na Kitunda ambao walikubali fidia ya kiasi cha shilingi 717 milioni zilizotengwa kupisha ujenzi wa mradi huo.
“Bado kuna wananchi wapatao 23 ambao hawajaridhia malipo ya fidia yao. TANESCO kamilisheni mazungumzo hayo haraka walipwe ili kupisha ujenzi uendelee, kwa sababu hatuwezi kusababisha watu zaidi ya elfu 10 kukosa umeme sababu ya watu 23. Nataka ifikapo tarehe 20 Januari Mkandarasi aendelee na kazi,”alisema Kalemani.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali ili kuwezesha miradi mbalimbali ya umeme kutekelezwa kutokana na umuhimu wa nishati hiyo kiuchumi. “Kama kuna wananchi wanazuia miradi ya umeme tupeni nafasi tufanye kazi, umeme ni uchumi na maendeleo”,aliongeza Dkt. Kalemani.
Pia, ameitaka TANESCO, kuhakikisha inaacha urasimu wa kukatwa kwa umeme hasa kipindi cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka za Christmas na mwaka mpya ili kuwafanya wananchi wapate huduma hiyo muhimu.
Naye, Mhandisi Mkuu wa Miradi, Frank Mashalo, kutoka TANESCO alieleza kuwa, kuchelewa kukamilika kwa wakati kwa miradi hiyo kumetokana na wananchi wa baadhi ya maeneo ya Mbagala kugomea malipo ya fidia.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja, akitoa majumuisho alieleza kuwa, ziara hiyo imesaidia kuona udhaifu wa utekelezaji wa miradi hiyo na hivyo aliahidi kuhakikisha kwamba mapungufu yote yanayafanyiwa kazi na kukamilika kwa mujibu wa maagizo na maelekezo ya Dkt. Kalemani.
Kwa upande wake Kamishna Masaidizi wa Nishati, anayeshughulia Maendeleo ya Nishati, James Andilile, alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utafuatiliwa kwa karibu ikiwemo kuhakikisha kwamba changamoto za mradi huo zinatafutiwa suluhisho la kutosha.
Gharama za ujenzi wa mradi huo ulioanza mwaka 2010 na kusainiwa mwaka 2012 ni Dola za Marekani milioni 34.2 ambapo tayari serikali imekwishalipa dola za Marekani milioni 28.
Mbali na Dar es Salaam, mradi wa kuboresha miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme wa (TEDAP) pia unatekelezwa katika mikoa ya Arusha, na Kilimanjaro.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani alifanya ziara ya kushtukiza katika ofisi ya TANESCO, Kinondoni Kusini ili kuona namna wananchi wanavyohudumiwa katika ofisi hizo na kuangalia utendaji kazi wa ofisi hiyo.