NA MICHAEL MAURUS.
KARIBUNI wasomaji wangu katika safu hii ambayo huwa inawajia kila Jumatatu, ikilenga kupashana hili au lile kuhusiana na masuala ya michezo na burudani.
Japo katika mada hii nimejitambulisha kama Kocha Mchezaji, lakini ni vema ikafahamika hilo halinizuii kujadili masuala mengine kama burudani kwani wapo ‘makocha’ wenzangu ambao huwa wanajihusisha na burudani, mfano mzuri akiwa ni kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali ambaye ni mkali wa muziki wa kizazi kipya.
Baada ya muda mrefu kujadili mambo ya soka, leo ninageukia tasnia ya urembo. Kwa wale wasiofahamu, mambo ya urembo nipo nayo karibu kwani nilishawahi kuibuka mwandishi bora wa Vodacom Miss Tanzania 2007 nikapata fursa ya kwenda Miss World nchini China kuripoti shindano la mwaka huo, nikiongozana na mrembo Richa Adhia.
Pia, nimekuwa jaji wa mashindano hayo kwa ngazi za vitongoji kwa takribani miaka minne, lakini pia kwa miaka mitano nimekuwa Jaji Mkuu wa kipengele cha michezo katika fainali za Miss Tanzania.
Kwa hayo, inatosha kunifanya kuwa miongoni wanafamilia wa mashindano hayo hivyo kuwa na haki ya kutosita kujadili suala lolote linalohusiana na tasnia hiyo.
Desemba 14, mwaka jana, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), lilitangaza kuyafungia mashindano ya Miss Tanzania kwa muda wa miaka miwili kutokana na kile kilichodaiwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu na sheria za uendeshaji wa mashindano hayo.Hatua hiyo ilionekana kuwashutua wengi kutokana na umaarufu wa mashindano hayo.
Binafsi sikutaka kukurupuka kuandika lolote badala yake niliamua ‘kuingia msituni kusaka ndondo’ za kutosha kuniwezesha kuwatendea haki BASATA, Lino International Agency ambao ndio waandaaji wa mashindano hayo pamoja na wadau wa urembo kwa ujumla.
Hatimaye nimefanikiwa katika hilo na leo nimeona ni vema nikatoa dukuduku langu ambalo naamini mwisho wa siku, wadau halisi wa urembo watapata majibu iwapo hatua hiyo ya kufungiwa kwa mashindano hayo ni sahihi au la.
Kutokana na ‘document’ nilizofanikiwa kuzipata baada ya kuhaha kwa muda mrefu, kuna mambo ambayo wadau wa urembo ningependa tuyatafakari kwa kina bila kujali itikadi zetu juu ya mashindano ya Miss Tanzania au uhusiano wetu na Mkurungezi wa Lino, Hashim Lundenga.
Kwa mujibu wa barua kutoka Basata kwenda Lino International Agency yenye kumbukumbu BST/PR/LIAL/VIII/14 ya Desemba 12, 2014 juu ya kufungiwa kwa mashindano ya Miss Tanzania, sababu iliyotolewa juu ya uamuzi huo ni kutokana na ‘ukiukwaji mkubwa wa taratibu na sheria za uendeshaji wa mashindano hayo.
Barua hiyo ilisomeka kuwa uamuzi huo umelenga kurejesha heshima katika tasnia ya mashindano ya urembo nchini na kwamba Baraza linaamini kuwa muda huu uliotolewa kwa Lino utatosha kujirekebisha na kujipanga upya.
Baraza hilo lilionya kuwa endapo kasoro zilizojitokeza hazitarekebishwa ndani ya kipindi hicho, halitasita kuendelea kuifungia Lino hadi hapo kasoro zote zilizobainishwa zitakaporekebishwa.
Barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, nakala yake ilitumwa kwa Katibu Mkuu WHVUM, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Sanaa la Taifa, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Wakurugenzi wa Maendeleo wa mikoa, ikiagizwa aione Afisa Utamaduni wa Mkoa na Wakurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya, ikiagizwa aione Afisa Utamaduni wa Wilaya.
Lakini kabla ya kufungiwa kwa shindano hilo, kuna barua ambayo Basata waliwaandikia Lino iliyotolewa Oktoba 7, mwaka jana yenye kumbukumbu no. BST/PR/LIALl/VOL. 7/159 ambayo iliwataka Lino kuwaondoa kambini warembo katika orodha ya ushiriki wa mashindano hayo ya taifa wale waliopatikana kutokana na mawakala ambao hawajasajiliwa na Basata, mpaka hapo watakaposajiliwa.
Kwa mujibu wa barua hiyo, kushindwa kufanya hivyo, hatua zifuatazo zitachukuliwa dhidi ya Lino ambazo ni kusimamisha shindano, kufungiwa shughuli za uendeshaji wa shughuli za sanaa kwa muda usiojulikana na kufutiwa usajili.
Baada ya barua hiyo, ilifuata nyingine ya Novemba 21 mwaka jana ambayo ilikuwa ikitoa onyo kali kwa Lino ikirejea maazimio ya kikao kati ya Lino na Basata cha Oktoba 3, 2014 katika ukumbi wa baraza hilo.
Barua iliyo ilisema kuwa Lino walikiuka kwa makusudi taratibu za baraza hilo kwa kuwatumia mawakala wasiosajiliwa, kuanza mchakato wa mashindano bila kuwa na kibali cha uendeshaji wa matukio, kutokuwasilisha mikataba ya washiriki wa mashindano kwa wakati na kutowasilisha taarifa za mashindano kwa wakati.
Mambo ya kujiuliza juu ya kufungiwa kwa mashindano hayo.
Barua ya kwanza ya Basata kwenda Lino Oktoba 7 takribani siku sita kama si tano kabla ya kufanyika kwa shindano, baraza hilo liliagiza warembo ambao mawakaal wao hawajasajiliwa waenguliwe. Je, ilikuwa ni halali kufanya hivyo kwa warembo ambao walishafanya maandalizi yaliyoambatana na kutumia fedha zao kujiandaa kwa shindano hilo?
Je, ingekuwa ni kuwatendea haki wadhamini ambao walitumia mamilioni yao kwa maandalizi ya shindano hilo kuwaengua warembo waliotajwa zaidi ya 10 kutokana na makosa ya mawakala wao ambao kimsingi wanawajibika moja kwa moja kwa Basata ambao ndio wanaotoa vibali?
Basata kwa kushirikiana na Lino walishindwa vipi kuwabana mawakala hao tangu ngazi za vitongoji? Kama walishindwa wote, kwanini lihukumiwe shindano pekee ikizingatiwa mara nyingi Basata huwa wanatuma wawakilishi wao katika mashindano ya vitongoji, ikiwa ni pamoja na kualikwa wakati wa semina za mawakala kuelekea mashindano hayo ya urembo?
Lakini baada ya shindano kufanyika, Basata waliitisha kikao cha tasmini ya mashindano hayo ambapo wajumbe kadhaa, akiwamo Kocha Mchezaji, walitoa mapendekezo yao juu ya kuboresha kasoro zilizojitokeza, ikiwamo suala la uwazi wa mikataba, uboreshaji wa zawadi na mashindano kwa ujumla. Kinachoshangaza, kwanini badala ya Basata kutoa nafasi kwa mapendekezo ya wajumbe kufanyiwa kazi na Lino, waliamua kulifungia shindano?
Lakini inakuwaje baraza hilo litoe onyo kwa Lino na siku chache baadaye wanalifungia shindano, nini maana ya onyo lao? Lakini hatua ya kufungia shindano kwa miaka mwili, limelenga katika kulijenga au kumkomoa mtu? Je uamuzi huo umewafikiria vipi mabinti ambao wamekuwa wakihaha huku na kule kusaka ajira bila mafanikio, wengine wakidiriki hata kujidhalilisha ili kupata ajira?
Leo hii tunawaona watu maarufu kama Wema Sepetu, Jokate Mwegelo, Faraja Kota, Nancy Sumari, Richa Adhia na wengineo ambao maisha yao yameboreka kwa kiasi kikubwa baada ya kutengeneza majina yao kupitia mashindano ya Miss Tanzania, Basata wanapolifunmgia shindano hilo, wamewafikiriaje mabinti wa kitanzia wenye ndoto za kufuata nyayo za akina Jokate au Nancy?
Naomba kwa leo niishie hapa nikitarajia kupata maoni ya wasomaji wa safu hii na wa urembo kwa ujumla ili wiki ijayo tuweze kuhitimisha mada hii.
Nawatakia wiki njema.