DSC07094
Aliyekuwa tabibu msaidizi wa Dispensari ya Tumaini mjini Singida, (wa mbele) Godlisten Raymond (37) na mfanyabiashara wa mbuzi na biashara ya kusaga nafaka (wa tatu mbele) Adamu Shaban Hole (46) mkazi wa kijiji cha Kitandaa tarafa ya Sepuka wilaya ya Ikungi,wakisindikizwa na askari polisi kwenda gerezani kuanza kutumikia adhabu ya kila mmoja kifungo cha miaka 10 baada ya kupatikana na hatia ya kumtoa mimba mwanafunzi na kusababisha kifo chake.
DSC07095
Mfanyabiashara wa Mbuzi na kusaga nafaka katika kijiji cha Kintandaa Adamu Shaban Hole (46) (mbele mwenye kofia baraghashia) na aliyekuwa tabibu msaidizi katika dispensari ya Tumaini mjini Singida, Godlisten Raymond (37) aliyefunika uso,wakisindikizwa gerezani kwenda kuanza kutumikia kifungo cha miaka 10 baada ya kutiwa hatiani na mahakama kuu kanda ya kati kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi na kuitoa na kusababisha kifo chake.Mwanafunzi huyo Hamida Athumani (16) alifariki dunia siku chache kabla ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.(Picha na Nathaniel Limu).7
Na Nathaniel Limu, Singida
MAHAKAMA Kuu kanda ya kati iliyomaliza vikao vyake hivi karibuni mjini Singida,imewahukumu aliyekuwa tabibu msaidizi wa dispensari ya Tumaini Godlisten Raymond (37) adhabu ya kutumikia jela miaka 10 baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kutoa mimba kwa njia isiyo sahihi kwa  mwanafunzi na kusababisha kifo chake.
Mshitakiwa Godlisten anadaiwa kumtoa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi Kintandaa tarafa ya Sepuka wilaya ya Ikungi, Hamida Athumani (16) septemba saba mwaka 2006 na alifariki dunia septemba 17 mwaka huo huo wa 2006, siku chache kabla ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Pia katika kesi hiyo,mfanyabiashara wa mbuzi na kusaga nafaka mkazi wa kijiji cha Kitandaa tarafa ya Sepuka wilaya ya Ikungi,Adamu Shabani Hole (46),naye amepewa adhabu ya kutumikia jela miaka 10 baada ya kupatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi Hamida Athumani (16) na kisha kushiriki kutoa mimba hiyo na kusababishia kifo mwanafunzi huyo.
Ilidaiwa mahakamanai hapo kuwa mshitakiwa wa pili ambaye ni mfanyabiashara ya mbuzi,Adamu,katika kipindi hicho hicho,aliweza kumpa mwanafunzi mwingine Rukia Juma aliyekuwa akisoma darasa moja na Hamida (marehemu).
Rukia baada ya kutolewa mimba na washitakiwa,aliweza kulazwa katika hospitali ya mkoa mjini hapa,na aliweza kunusurika kufariki dunia baada ya kupatiwa matibabu.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo,mwendesha mashitaka wakili wa serikali mkuu mfawidhi kanda ya Singida,Neema Mwanda,aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali ya kifungo cha maisha jela kwa washitakiwa,ili iwe fundisho kwao na watu wengine wanaotarajia kuwatoa mimba wasichana wadogo na kisha kusababisha vifo vyao.
“Vitendo vya watu wazima kufanya mapenzi na wanafunzi na kisha kuwapa ujauzito,havikubaliki kabisa,kwa sababu zinaharibu maisha ya wanafunzi husika na wakati mwingine vinasababisha vifo.Pia madaktari na tabibu wasaidizi wenye tabia ya kutoa mimba kwa njia isiyo salama,nao wanakwenda kinyume na sheria za taaluma zao”,amesema Mwanda.
Kwa upande wake wakili wa kijitegemea kutoka Dodoma mjini.Deus Nyabiri aliyekuwa anamtetea mshitakiwa wa kwanza,Godlisten,aliiomba mahakama hiyo impe adhabu nafuu mteja wake ikizingatia kuwa kosa hilo ni la kwanza kwake na pia anategemewa na familia yake na ya wazazi wake ambao kwa sasa,wana umri mkubwa.
Naye wakili wa kujitegemea wa mjini hapa,Raymond Kimu aliyekuwa akimtetea mshitakiwa wa pili,Adamu,aliiomba mahakama hiyo impe adhabu nafuu mteja wake na kiwezekana imwachie huru,kwa madai kuwa baada ya kuwapa mimba wanafunzi wawili waliokuwa darasa la saba,mke wake amemkimbia na familia yake imemtega.
Akitoa adhabu hiyo,jaji Cresentia  Makuru, amesema kwa mazingira ya kawaida,kosa walililofanya  washitakiwa,hawastahili huruma ya mahakama.
Amesema vitendo vya wasichana wadogo kupoteza maisha kwa kutolewa mimba kwa njia isiyo salama,licha ya kusababisha vifo vyao,pia vinachangia ndoto za wazazi kwa watoto wao,kupotea.
Aidha,jaji Makuru amesema katiba ya nchi,inatamka wazi kwamba uhai wa mtu ni lazima uheshimiwe na kulindwa.Hata sheria za kimataifa nazo zimetamka hivyo hivyo.