Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.
MBUNGE wa Kigoma mjini Zitto Kabwe, leo Novemba 2, 2018 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi.
Mashtakia Zitto amesomewa mashtaka yake na wakili wa serikali Mwandamizi, Tumain Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi.
Wakili Kweka amedai Oktoba 28, 2018 akiwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya ofisi ya chama cha ACT Wazalendo mshtakiwa Zitto akiwa katika mkutano huo kwa nia ya kuleta chuki kwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la polisi alitoa Maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.
Katika shtaka la pili, Kweka alidai kuwa siku na mahali hapo, Zitto Kijitonyama alitoa Maneno ya uchochezi ambayo y yalikuwa na lengo lenye kuleta hofu.Aidha Zitto anadaiwa Kutoa walaka kwa umma ukiwa na Maneno ya kichochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa watanzania dhidi ya polisi.Hata hivyo, mshtakiwa amekana mashtaka hayo amachiwa huru kwa dhamana na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Hata hivyo Wakili Kweka amewasilisha hati ya kiapo iliyoapwa na mkuu wa Upelelezi wa Kipolisi Mkoa wa Kinondoni SSP John Malulu ya kupinga dhamana dhidi ya Zitto.Katika hati hiyo ya kiapo wanaiomba mahamakama isitoe dhamana kwa mshtakiwa kwa sababu za kiusalama, na kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, Amedai iwapo mshtakiwa huyo ataachiwa kwa dhamana ataweza kuingilia upelelezi.
Wakili Peter Kibatala anayemtetea Zitto ameiomba mahakama impatie dhamana mteja wak na kwamba hati ya kiapo iliyowasilishwa na upande wa mashtaka mahakamani hapo inamapungufu ya kisheria ikiwamo kuwa hati ya kiapo haitakiwi kutajwa vifungu vya sheria.Kibatala alieleza kuwa hata kama kuna hati ya kiapo mahakamani, hakuna sababu za msingi zilizotolewa kuishawishi mahakama kumnyima dhamana Kabwe.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Shahidi amesema katika hati ya kiapo iliyowasilishwa na upande wa mashtaka ni lazima iwepo na sababu za kutosha na za msingi kupinga dhamana.Amesema ni jukumu la polisi kulinda raia na Mali zao kwa hilo nashangaa polisi kuhofia usalama wa Zitto wakati ni jukumu lao kuhakikisha kila RAIA kuwa salama."Ni kweli hati ya kiapo imebeba vifungu vya sheria wakati siyo matakwa ya sheria kwa namna hiyo sowezi kumnyima dhamana.
Hivyo Hakimu Shahidi amemtaka Zitto kuwa na mdhamini mmoja Mwenyekiti kitambulisho atakayesaini bondi ya Sh 10 milioni.
Zitto amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana na kuachiwa huru na kesi imeahirishwa hadi Novemba 26, mwaka huu.
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe akifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kushikiliwa katika kituo cha Polisi kwa siku kadhaa. Mh. Zitto ameachiwa kwa dhamana ya mdhamini mmoja na bondi ya sh. Milioni kumi
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, akiwa katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akisubiri kusomewa mashtaka yake yanayomkabili. Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi.
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, akiteta jambo na wakili wake Steven Mwakibolwa, kabla ya kwanza kusomewa kwa kesi hiyo katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.