Na Veronica Kazimoto ,Dar es Salaam
Hivi karibuni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ilitoa msamaha maalum wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 tofauti na asilimia 50 ya hapo awali.
Msamaha huu umetokana na malalamiko ya wafanyabiashara waliyoyatoa kwa Mhe. Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli ya kuwepo kwa malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma yakijumuisha riba na adhabu wakati wa Mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 19 Machi, 2018.
Kufuatia malalamiko hayo, Rais aliwaambia wafanyabiashara hao kuzungumza na Wizara ya Fedha na Mipango ili waweze kupunguziwa riba na adhabu za madeni yao ya kodi.
"Suala la kodi ni very sensitive (nyeti sana) hata Rais unaweza kushtakiwa kwa kukwepa kodi, mimi niwaombe wale mnaodaiwa kwa miaka ya nyuma nendeni mka-negotiate (mkajadiliane) na Wizara ya Fedha, ninajua kuna kipengele ambacho kinaweza kuwapunguzia", alisema Rais Magufuli.
Dk. Magufuli alitumia baraza hilo pia kuwasisiza wafanyabiashara kulipa kodi ambapo alisema "Tunahitaji kodi kwa ajili ya survival (kudumu) ya nchi hii, mtu ajue kwamba kulipa kodi ni wajibu wake na kukwepa kodi is a big crime (kosa kubwa). Hivyo ninawaomba wafanyabiashara msikwepe kulipa kodi, mjitahidi kulipa kwa maana kodi hizi ndio zinatusaidia kuijenga nchi yetu".
Baada ya mkutano huo wa baraza la biashara, Bunge la Tanzania katika kikao chake cha bajeti cha Mwaka wa Fedha 2018/19 cha mwezi Juni, 2018 lilipitisha marekebisho ya Kifungu cha 70 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 ili kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Fedha ya kutunga kanuni maalum za kutoa msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi ya nyuma.
Kupitia marekebisho hayo, Waziri wa Fedha na Mipango, alimpa Mamlaka Kamishna Mkuu wa TRA kutoa msamaha maalum wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 tofauti na asilimia 50 ya awali.
Ni kufuatia mamlaka hayo, Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere alitangaza msamaha huo maalum mnamo tarehe 11 Julai, 2018 kwa lengo la kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni ya riba na adhabu kwa kuwapa fursa ya kulipa kodi ya msingi (principal tax) mara moja au kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha wa 2018/19.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu Kichere alisema kuwa msamaha wa riba na adhabu unahusu kodi zote zinazotozwa kwa mujibu wa Sheria zinazosimamiwa na TRA ambazo ni Sheria ya Kodi ya Mapato sura. 332, Kodi ya Uendelezaji Ufundi Stadi sura 82, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani sura 148; Sheria ya Ushuru wa Stempu sura 189, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura 147, Sheria ya Ada ya Huduma za Bandari sura 264 pamoja na Sheria ya Ada ya Huduma ya Viwanja vya Ndege sura 365.
Hivyo basi, mapato yasiyo husika na utaratibu huu ni yale yasiyo ya kodi ambayo TRA imepewa jukumu la kisheria la kukusanya kwa niaba ya Serikali za Mitaa, Wakala na Taasisi za Serikali. Mapato hayo ni kama vile Kodi katika Michezo ya Kubahatisha, Kodi za Majengo, Tozo ya kuendeleza utalii, Tozo ya kuendeleza Reli na Ada za Matangazo.
Aidha, katika mkutano huo wa waandishi wa habari, Kamishna Mkuu Kichere aliwataja walengwa wa msamaha huu ambapo alisema "Walengwa wa msamaha huu ni makampuni, taasisi na watu binafsi ambao wamewasilisha ritani ya kodi lakini bado wanadaiwa kodi yote au sehemu ya kodi zitokanazo na ritani hizo, hawajawasilisha ritani za kodi, hawajasajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) au Namba ya Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na wale walio wasilisha pingamizi au rufaa za kodi ambazo bado zinashughulikiwa katika ofisi za TRA, Bodi ya Rufaa na Mahakama ya Rufani za kodi".
Pia, alitaja makampuni, taasisi na watu binafsi ambao hawahusiki na msamaha huu kuwa ni wale ambao wangestahili kupata msamaha lakini tayari wameshalipa madeni yao, masuala yao ya kikodi yapo katika hatua ya ukaguzi au uchunguzi, wana madeni ya nyuma ya kodi ambayo yanatokana na kesi za jinai za kodi, utakatishaji fedha, usafirishaji wa binadamu au shughuli nyingine haramu kama ilivyothibitika kisheria, wenye madeni ya nyuma ya kodi yanayotokana na adhabu zilizoamuliwa tayari au adhabu za makosa yatokanayo na uzembe wa kukusudia uliobainika kisheria pamoja na wenye riba au faini zilizotokana na kutoa au kutumia risiti za kielektroniki za kughushi.
"Mlipakodi atastahili kupata msamaha wa riba na adhabu endapo yeye binafsi au mwakilishi wake aliyeidhinishwa kisheria atawasilisha maombi ya msamaha kwa kutumia fomu maalum zinazojulikana kama ITX207.01.E zinazopatikana katika Ofisi za TRA mikoa yote au katika Tovuti ya TRA www.tra.go.tz na maombi yawasilishwe kwa Meneja wa Mkoa TRA au kwa Kamishna wa Walipakodi Wakubwa sambamba na kujaza Dodoso maalum la msamaha na ritani ya taarifa za mlipakodi,” alieleza Kichere.
Kichere aliongeza kuwa, mwisho wa kuwasilisha maombi hayo ni tarehe 30 Novemba, 2018 ambapo Ofisi ya Kamishna Mkuu wa TRA itajibu kwa maandishi maombi ya msamaha huo ndani ya siku thelathini (30) tangu siku ya kupokea maombi.
Lakini malipo ya kodi ya msingi baada ya kuondoa malimbikizo ya riba na adhabu yanaweza kufanyika mara moja au kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha 2018/19 na mwisho wa malipo hayo ni tarehe 30 Juni, 2019.
"Msamaha huu maalum umetolewa kwa walipakodi kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia tarehe 1 Julai 2018 mpaka tarehe 31 Desemba 2018 na madeni yanayohusiana na msamaha huu ni yale yote yaliyolimbikizwa hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2018 isipokuwa madeni ya wafanyabiashara wapya ambao hawajasajiliwa kama walipakodi,” alifafanua Kichere.
Ikumbukwe kwamba, mnufaika wa msamaha huu anapaswa kuwasilisha ritani zote ambazo hazikuwahi kuwasilishwa, kuingia mkataba wa makubaliano maalum na Kamishna Mkuu wa TRA utakaoanisha deni lote la kodi, riba na adhabu inayosamehewa na jinsi ya ulipaji wa kodi ya msingi kabla ya tarehe 30 Juni, 2019. Kodi ya msingi italipwa kwa mujibu wa masharti na taratibu za mkataba wa malipo na kwa mtu binafsi au taasisi ambayo ilikuwa ikifanya biashara au shughuli za uwekezaji lakini haijasajiliwa kama mlipakodi, itabidi isajiliwe kabla ya tarehe 30 Novemba, 2018.
Hata hivyo, msamaha utatolewa kwa maombi yatakayokidhi vigezo vya masharti na kukubaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo Kamishna Mkuu wa TRA na Mlipakodi husika watasaini mkataba wa makubaliano utakaoainisha deni lote la kodi, riba na adhabu inayosamehewa, pamoja na kodi isiyo na riba wala adhabu itakayopaswa kulipwa kabla ya tarehe 30 Juni, 2019.
Kutokana na umuhimu wa msamaha huu, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na zoezi la kutoa semina elekezi kwa wafanyabiashara, washauri wa wafanyabishara (tax consultants) na wadau mbalimbali kote nchini ili waweze kuwasilisha maombi yao kwa usahihi na hatimaye kunufaika na msamaha husika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa semina hizo uliofanyika katikati ya mwezi Agosti, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa wa Mamlaka hiyo Alfred Mregi alisema kwamba TRA ina jukumu la kuhakikisha kuwa, wafanyabiashara wengi wanajitokeza kwa wingi kuomba msamaha wa riba na adhabu ili waweze kunufaika na msamaha huo maana wamekuwa wakilalamikia suala hili kwa muda mrefu.
"Mtakumbuka kwamba, wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiomba kupunguziwa riba na adhabu ya malimbikizo ya kodi kwa muda mrefu. Malalamiko haya yalifikishwa hadi kwa Mhe. Rais ambaye alitoa maelekezo ya kutoa msamaha huu. Hivyo, sisi kama TRA tuna jukumu la kupeleka habari hii njema kwa wafanyabiashara wote ili wajue kwamba maombi yao yalipokelewa na sasa wanaweza kupata msamaha wa riba na adhabu kwa asilimia 100," alisema Mregi.
Uzinduzi wa semina hizi elekezi ulihudhuriwa na wafanyabiashara wapatao 500 ambapo mmoja wa wafanyabiashara wakubwa kutoka kampuni ya Super Group of Companies inayozalisha Sukari ya Mtibwa na Kagera Ibrahim Ali alimshukuru Rais Magufuli kwa kupokea na kufanyia kazi malalamiko yao ya muda mrefu lakini pia hakusita kuishukuru TRA kwa kutoa semina elekezi ambayo imewasaidia kuelewa mambo mengi kuhusiana na msamaha huo.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Ali alisema "Kwa kweli mimi napenda kumshukuru Rais Magufuli kwa kusikia kilio chetu sisi wafanyabiashara na napenda pia kuishukuru TRA kwa kuanzisha programu hizi za kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuongeza uelewa na namna bora ya kuwasilisha maombi ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi, alieleza Ali.
Mpaka sasa, semina hizi elekezi zinaelendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini na licha ya kutoa elimu hii kupitia semina, TRA inajitahidi kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii pamoja na kukutana na wafanyabiashara, washauri wa wafanyabiashara na wadau mbalimbali katika majukwaa na mikutano ya mabaraza ya biashara ngazi ya mkoa na wilaya.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Richard Kayombo ambaye ndiye anayeongoza gurudumu hili la kutoa elimu hii kuhusu msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi pamoja na elimu ya kodi kwa ujumla, amekuwa akiwahimiza walipakodi kutumia fursa hii adhimu ili waweze kuondokana na malimbikizo ya madeni na hatimaye waweze kulipa kodi ya msingi pekee.
Akizungumza wakati wa Jukwaa la Fursa za Biashara lililofanyika mwezi Agosti, 2018 mkoani Geita, Mkurugenzi Kayombo alisema "Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara wote wenye malimbikizo ya madeni ya kodi na wote waliokuwa wakifanya biashara bila kusajiliwa kuwasilisha maombi yao TRA ili waweze kupata msamaha huu wa riba na adhabu kwa asilimia 100 ambapo mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Novemba, 2018."
Aidha, Kayombo aliwaambia washiriki wa jukwaa hilo kuwa wasisite kuwasiliana na Mamlaka pale watakapohitaji msaada zaidi juu ya zoezi hili kwa kutembelea Ofisi za TRA zilizopo nchi nzima, kutembelea tovuti ya TRA www.tra.go.tz au Kituo cha Huduma kwa Mlipakodi kinachopatikana kwa namba za simu za bure 0800 750 075 au 0800 780 078 au kutuma barua pepe huduma@tra.go.tz.
Kazi kwenu walipakodi, kile mlichokuwa mkikililia kwa muda mrefu mpaka kufikisha malalamiko yenu kwa Mhe. Rais kimefanyiwa kazi, hii inaonyesha kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu na inatekeleza ahadi zake kwa vitendo. Chamgamkieni fursa hii mapema kabla muda uliopangwa wa kutuma maombi haujaisha ili muweze kunufaika na msamaha huu wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitangaza msamaha maalum wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 jijini Dar es Salaam Julai, 2018. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka hiyo Richard Kayombo.