Na James Festo.Makete
Jeshi la polisi nchini limeaswa kutenda kazi kwa haki bila kushurutishwa na mtu yeyote kwani lisipofanya hivyo haki haitatendeka kwa kila raia kama katiba inavyosema kusababisha maafa mbalimbali yatakopelekea kuvinjika kwa amani
Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Makete Shaaban Mkakanze wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ivalalila wilayani hapa waliojitokeza kumpokea mwenyekiti wa CHADEMA kijijini hapa aliyekuwa gerezani mara baada ya kuachiwa huru.
"jeshi la polisi ni zuri sana pale litakaposimamia haki, lakini wanapokwenda kinyume kwa kweli wanageuka mwiba mchungu kwa wananchi" alisema Mkakanze.
Mkakanze amesema hukumu iliyotolewa na mahakama ya mwanzo makete mjini Juni 28 mwaka huu dhidi ya mwenyekiti huyo imeonekana kuwa na mapungufu mengi ambayo amesema atayataja katika mkutano wa hadhara utakaofanyika muda wowote kuanzia sasa, hivyo ndiyo maana wameibuka kidedea katika rufaa waliyokata.
Amesema wao kama chama hawatakatishwa tamaa na mambo kama hayo na badala yake wataendelea kupigania haki za wananchi pale wanapoonewa na ikibidi hata kupoteza maisha wakati wakipigania haki zao
"Chadema sisi si watu wa vurugu, lakini sisi tunasimamia haki na maendeleo ya wananchi bila kujali itikadi za vyama, hata yeyote tupo pamoja nae kama anatenda haki na kile anachotakiwa kuwafanyia wananchi lakini anapokwenda kinyume sisi hatutakubali na badala yake tutapambana mpaka kieleweke" alisema Mkakanze
Naye mwenyekiti wa CHADEMA kijiji cha Ivalalila ambaye alikuwa gerezani Bw Godfrey Mahenge amesema hana cha kusema zaidi ya kumshukuru Mungu na wananchi wa kijiji hicho ambao walikuwa naye pamoja tangu wakati wa kesi hadi gerezani na kusema kwa sasa ametoka na wembe ni ule ule wa kupigania haki za wananchi wake
Amesema kwa sasa hana mengi ya kuongea zaidi atakuja kuzungumza kwenye mkutano wa hadhara ambao utaandaliwa kwa ajili ya wananchi hao ambapo anatarajia kueleza yote yaliyomkuta ili wananchi wake wajue, huku akitoa rai kwa waandishi wa habari kuutangazia umma kuwa hivi sasa yuko huru na kesi zote ameshinda kama ilivyokuwa wakati akitiwa nguvuni.
"Nawaomba waandishi wa habari kama mlivyotangaza wakati nafungwa naomba mtangaze pia na jinsi nilivyoshinda rufaa na kuwa huru" alisema Mahenge
Mnamo Juni 28 mwaka huu mahakama ya mwanzo makete mjini ilimtia hatiani kwa kosa la kutukana polisi hivyo kuhukumiwa kifungo cha miezi 9 gerezani hali iliyomlazimu kukata rufaa na kushinda rufaa hiyo na alikaa jela zaidi ya miezi miwili