Na Dixon Busagaga, Moshi
KESI ya tuhuma za mauaji ya kukusudia linalomkabili mmilikiwa wa Shule ya Sekondari ya Scolastica Edward Shayo na wenzake wawili limehairishwa kwa mara ya tatu sasa na sababu ya kuahirishwa ikitajwa imetokana na kuharibika kwa gari la kubebea mahabusu.
Kwa jana kesi hiyo ilipangwa kuendelea kwa hatua ya usomaji wa maelezo ya mashahidi kwa ajili ya kufunga ushahidi kabla ya shauri hilo kuhamishiwa Mahakama Kuu. Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Sophia Masati alieleza kuwa shauri hiyo itatajwa kwa ajili ya usomaji wa maelezo ya mashahidi Agosti 3,mwaka huu.
“Kesi hii imeahirishwa hadi Agosti 3 mwaka huu kwa ajili ya kuja kusoma maelezo ya mashahidi wa kesi hii,"amesema Hakimu huyo.Kabla ya kutajwa kwa mara nyingine kwa shauri jana, Julai 6 mwaka huu Hakimu mkazi wa mahakama ya hakimi mkazi ,Moshi ,Julieth Mawole aliieleza maelezo ya ushahidi wa shauri hilo utatolewa .
Kwa mara ya kwanza usomaji wa maelezo ya kufunga ushahidi uliahirishwa baada ya washtakiwa kushindwa kufikishwa mahakamani.Sababu za kutofika kwa washtakiwa mahakamani hapo zilitajwa kuwa ni mkanganyiko wa tarehe iliyopangwa na mahakama hiyo ambayo ilikua ni June 29 mwaka huu kutofautiana na ile iliyowasilishwa Mahabausu Gereza la Karanga ambayo ilitajwa kuwa ni Julai 29 ,mwaka huu.
Maelezo hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali,Agatha Pima alipoomba kupangwa kwa tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea kwa hatua ya Kufunga Ushahidi kwenda Mahakama kuu.Ombi hilo lilipingwa na Wakili wa upande wa utetezi anaye mtetea Mshtakiwa wa Pili katika shauri hilo ,Edward Shayo,Elikunda Kipoko akieleza kutoridhishwa na maelezo ya upande wa Jamhuri .
Hata hivyo Hakimu,Mawole aliarisha Shauri hilo na kuoanga Julai 6 mwaka huu huku akieleza kusikitishwa na kitendo hicho kwa Washtakiwa kushindwa kufikishwa mahakamani hapo kutokana na mkanganyiko huo wa tarehe .Julai 6 mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi ,Moshi ilihairisha kuendelea na shauri kwa mara nyingine safari hii sababu zikitajwa ni kuugua ghafla kwa wakili wa upande wa Jamhuri ,Agatha Pima muda mfupi kabla ya kuanza kwa shauri hilo.
June 27,mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi ,Moshi ilielezwa kukamilika kwa upelelezi wa shauri hilo linalomkabili mmiliki wa shule ya sekondari ya Scolastica,Edward Shayo na wenzake ,Laban Nabiswa(Mwalimu) na Hamisi Chacha,mlini wa shule hiyo.
Wakili wa serikali Agatha Pima aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo la mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi Humphrey Makundi umekamilika kwa asilimia 100.
Novemba 6,mwaka jana Mwanafunzi huyo ,mwili wake ulikutwa umetupwa mto Ghona mita 300 kutoka eneo la shule hiyo ambapo mwili huo ulizikwa katika makaburi ya Manispaa ya Moshi Novemba 12,mwaka jana.