Na Rhoda Ezekiel Kigoma,
HALMASHAURI ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge wameandaa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo wilayani humo.
Lengo ni kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuongeza uelewa kwa wajasiriamali katika shughuli wanazofanya.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo jana wilayani Buhigwe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Anosta Nyamoga amesema semina hiyo inamalengo matatu , moja ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ili kuwawezesha na kuwapa mafunzo wajasiriamali wadogo wadogo.
Pia kuongeza mapato kwa halmashauri kwakuwa wajasiriamali wakiongeza kipato hata pato la halmashauri linaongezeka kupitia ukusanyaji wa kodi na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema asilimia kubwa ya mapato ya Wilaya ya Buhigwe yanategemea ukusanyaji wa ushuru wa mazao na kodi kutoka kwa wajasiriamali wadogo , semina hiyo ya kuwajengea uwezo wajasiriamali na kufaungua masoko ya nje ya nchi kwa kuwajenga wananchi kutengeneza bidhaa zenye ubora na kutumia masoko ya ujirani mwema kuuza bidhaa zao na kuongeza kipato chao itasaidia uchumi kuongezeka.
Amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 walikusanya shilingi milioni 450 , na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 wamekusanya milioni 550 na Malengo ya Wilaya hiyo ni kufikia kukusanya kiasi cha Sh bilioni moja ifikapo 2020 kutokana na Miundombinu ya biashara kuboresha na kukamilika kwa soko la ujirani mwa litakalo jengwa Manyovu, ambapo wanatarajia kukusanya zaidi ya milioni 100 kupitia soko hilo.
" Wilaya ya Buhigwe tumejipanga ipasavyo kuhakikisha Wananchi wetu wanatoka kwenye maisha waliyokuwa nayo ya kufanya biashara kwaajili ya kupata chakula kwa sasa tunataka waanze kufanya biashara kwa malengo zaidi kwakuwa fursa ni nyingi na Wananchi walikuwa hawazitumii tunaamini kupitia semina hii uchumi utaongezeka na manufaa watayaona", alisema mkurugenzi huyo.
Awali akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Brigedia Jenerali Marco Gaguti, aliwataka wafanyabiashara hao kutumia Mafunzo hayo kuongeza uwelewa na uzalishaji kwakuwa serikali imejipanga kumuwezesha kila mwananchi na Nchi kwa ujumla kufika uchumi wa kati.
Aidha amewataka kutumia fursa ya somo la Nje kwakuwa vizuizi vilivyo kuwepo vimeondolewa na serikali inamkakati wa kuifungua Wilaya hiyo na mikoa mingine kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji, watumie fursa hiyo kuzalisha mazao ya kutosha na kuongeza thamani mazao yao iliuchumi wao uendele zaidi.
" Wilaya yetu tunependelewa zaidi tuko mpakani mwa nchi tatu Burundi, Congo na Rwanda ninaamini wananchi wakitumia fursa hii Vizuri ninahakika uchumi wa Wananchi wetu utaongezeka na tutaifungu Wilaya ya Buhigwe ambayo ilikuwa nyuma tumeanza kwa semina hii ninaamini Wafanya biashara hawatakuwa vile walivyo watainuka zaidi", amesema Brigedia Gaguti.
Kwa upande wa Mbunge wa Manyovu Albart Obama amesema changamoto aliyokuwa akiipata kwa wawekezaji waliokuwa wakitaka kuja kuwekeza katika Wilaya hiyo ni pamoja na kukosekana kwa Umeme.
Amesema kwa sasa umeme umefika na masoko ya ujirani mwema yanajengwa anewaomba wawekezaji kuanzisha viwanda vya juisi na usindikaji kwakuwa Wilaya hiyo inayozalisha matunda mengi, kahawa pamoja na ndizi.
Obama amesema mafunzo hayo yataleta msukumo mpya kwa wananchi wa Buhigwe kutumia fursa kwa kujua namna ya kuongeza ubora na thamani ya mazao wanayo zalisha na kuinua uchumi wao kwa namna bora ya uwekezaji na kutumia masoko ya ujirani mwema kama chachu ya maendeleo kwao.
Naye Mfanyabiashara Leonardi Kataga amesema biashara ya Kahawa ndio wanayoitegemea kama wafanya biashara zao hilo likipatiwa soko na kuongezewa uthamani wanahakika zao hilo linaweza kuinua uchumi wao haraka na kuomba Serikali kuwasaidia katika zao hilo iliwaweze kuzalisha kwa Wingi.
Amesema wananchi wamefurahia na hatua ya Serikali kuwapatia mafunzo na kuongeza kuwa mafunzo hayo ni chachu kwao kuwafanya waendelee mbele.Pia wataweza kuongeza thamani katika uzalishaji na kutumia fursa zilizopo kuongeza kipato chao.
Baadhi ya Wajasiriamali Wadogo wakifuatilia mafunzo yaliyokuwa yakitolewa ukumbini humo mapema jana,mafunzo hayo yaliandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Manyovu .Lengo la mafunzo hayo ikiwa ni kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuongeza uelewa kwa wajasiriamali katika shughuli wanazofanya.