Quantcast
Are you the publisher? Claim or contact us about this channel


Embed this content in your HTML

Search

Report adult content:

click to rate:

Account: (login)

More Channels


Showcase


Channel CatalogChannel Description:

Karibuni Jamvini Wanajamii

older | 1 | .... | 1496 | 1497 | (Page 1498) | 1499 | 1500 | .... | 1904 | newer

  0 0

  Muonekano wa leo wa tuta la kutandazia reli ya kisasa (Standard Gauge) katika eneo la Soga mkoa wa Pwani takriban kilomita 37 kutoka Pugu mkoa wa Dar es salaam ulivyo sasa, ikiwa ni hatua iliyofikiwa katika muendelezo wa ujenzi wa reli hiyo ulioanza  mwezi Desemba mwaka jana katika mradi unaotarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu na utajengwa kwa awamu nne. 

  Kampuni Hodhi ya rasilimali za reli nchini (RAHCO) ndiyo inatekeleza mradi huo kutoka Dar es salaam kwenda Isaka na Mwanza imegawanyika katika awamu ndogo nne ikiwemo Dar es salaam hadi Morogoro, Morogoro hadi Makutupora, Makutupora hadi Tabora na Tabora hadi Mwanza. 

  Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa RAHCO Injinia Masanja Kadogosa jumla ya makandarasi  wanne wanaendelea na kazi usiku na mchana ili kukamilisha  ujenzi wa reli hiyo yenye upana wa mita 1.345 na ambao utaruhusu treni kutembea kwa spidi ya kilomita 160 kwa saa. 

  Mradi huu mkubwa unatarajiwa  kuchochea maendeleo katika sekta ya kilimo, biashara, madini na viwanda hususan maeneo ambapo reli hiyo itapita ikiwemo  nchi  jirani ya Rwanda ambayo imekubali kujenga aina hiyo ya reli toka Isaka hadi Kigali. Mtandao mzima wa reli nchini unaotegemewa kujengwa kwa kiwango cha standard Gauge una jumla ya kilometa 2,561 ukitarajiwa kugharimu Dola za Marekani Bilioni 7.6i Bilioni 7.683.  
   Eneo la Soga mkoa wa Pwani takriban kilomita 37 kutoka Pugu mkoa wa Dar es salaam
   Tuta linavyoonekana katika eneo la Soga mkoa wa Pwani takriban kilomita 37 kutoka Pugu mkoa wa Dar es salaam
   Sehemu ya tuta la kupitishia reli eneo la Soga mkoa wa Pwani takriban kilomita 37 kutoka Pugu mkoa wa Dar es salaam
   Sehemu ya tuta la kupitishia reli eneo la Soga mkoa wa Pwani takriban kilomita 37 kutoka Pugu mkoa wa Dar es salaam

  0 0

   Na Sultani Kipingo wa Globu ya Jamii

  Wanafunzi waandamizi saba wa  shule za Karate (dojo) mtindo wa Okinawa Goju Ryu  za  Kaizen na Hekalu la Kujilinda  za jijini Dar es salaam na Dodoma wamefanya mitihani na kufaulu kupandishwa madaraja ya mkanda mweusi chini ya Sensei Rumadha Fundi  (BOFYA HAPA KUMJUA) usiku wa Jumatatu Januari 22, 2018.
  Wanafunzi hao kutoka Kaizen dojo  iliyopo Shule ya Sekondari ya Jamhuri na dojo dada ya Hekalu la Kujilinda iliyopo katika shule ya msingi ya Zanaki ni pamoja na ma-Senpai Yusuf Kimvuli, Abdulwahud Aghfoul, Bilali Mtenga na Seif Soud ambao wamepanda kutoka mkanda mweusi daraja la kwanza (1st Dan)  kwenda la daraja la pili (2nd Dan) lijulikanalo kama "Nidan".
  Wakati ma-Senpai Kimvuli, Maghfoul na Mtenga wanatoka dojo la Kaizen, Senpai Seif Soud anatoka Hekalu la Kujilinda.
  Wanafunzi wengine watatu waliofaulu na kupanda daraja la kwanza (1st Dan) ama "Shodan" kutoka mkanda wa kahawia ni ma-Senpai Abdulmajid Khan wa Hekalu la Kujilinda pamoja na  Shaaban Yusuf na Galant Swai ambao wanatoka katika tawi la Hekalu la Kujilinda lililopo mjini Dodoma kwa jina la Miyagi dojo.
  Hii ni mara ya kwanza kwa  Sensei Rumadha Fundi  mwenye Dan 4,“Yondan” na  mwenye uzoefu mkubwa wa  mafunzo ya Goju Ryu chini ya walimu wakuu wengi maarufu toka Okinawa, Japan, kuwafanyia mitihani na kuwapandisha madaraja wanafunzi wa Tanzania.
  Sensei Rumadha, ambaye alianza mafunzo ya Okinawa Goju Ryu miaka 38 iliyopita  katika Hekalu la Kujilinda la Zanaki amesema anajisikia furaha na fahari kutimiza hilo jukumu lake kwa mara ya kwanza, na kwamba hajutii kufunga safari hii kutoka Houston, Marekani, anakoishi na kuja kuwasaidia ndugu zake.
  Na hilo liliwezakana baada ya mwaka jana huko  nchini Poland  Sensei Rumadha kufanya  na kufaulu vizuri mitihani wake wa kupanda ngazi toka Dan ya tatu "Sandan" kwenda ngazi ya nne "Yondan"  chini ya waamuzi (masters) toka Okinawa wakiongozwa na Sensei Yoshihiro Kancho Miyazato, ambaye ni Master au mwalimu mkuu wa Okinawa Goju Ryu Jundokan So Honbu Karate-Do huko Okinawa.
  Tokea hapo Sensei  Rumadha amekuwa na mamlaka ya kuwasaidia wanafunzi wake wa Tanzania na kuwafanyia mitihani na kuwapa wanafunzi  "Dan" hadi ngazi ya pili " Nidan" sababu katika Goju Ryu Karate  kuanzia Dan ya 3 na kuendelea hutolewa na Master Miyazato pekee.
  "Hawa waliofaulu na kupanda daraja la pili hivi sasa wana mamlaka ya kufungua shule zao chini ya uangalizi wangu na wakiendelea kufanya vyema nitatoa idhini ya wao kuwa waalimu ("Sensei") wanaotambulika Okinawa  baada ya muda si mrefu ujao" amesema Sensei Rumadha.
  Hakusita kutoa shukran zake nyingi kwa mlezi wake wa mafunzo tokea utotoni,  "Sensei Magoma Nyamuko Sarya akisema chini ya uongozi wake kitengo cha watoto kilichoitwa "Bomani Brigade"  kilichobuniwa  na mwanzilishi wa Okinawa Goju Ryu nchini Tanzania mwaka 1973,  hayati Sensei Nantambu Camara Bomani. 
  Alitoa shukurani za pekee kwa viongozi wa sasa wa Hekalu la Kujilinda - Sensei Mohamed Murudker, Sensei Wilfred Melkia, Sensei Geofrey Sawayael “Shoo” na Sensei Rashid Almasi ambao amesema moyo wao wa  kuendeleza Goju Ryu bila kutetereka pale Zanaki ni wa kusifika, na kwamba anawapongeza sana.
  Sensei Rumadha pia ameeleza kuwa kabahatika mwaka huu kualikwa kuiwakilisha Tanzania ambayo pamoja na na Angola ni nchi pekee za Afrika zilizoalikwa kuhudhuria maadhimisho ya miaka 65 tangu kuanzishwa kwa chama cha "Jundokan" na Master Eiichi Miyazato Sensei huko Naha City, Okinawa, mwezi wa Novemba 1918. 
  Chama hicho kwa sasa kinaongozwa na mwanawe Yoshihiro Kancho Miyazato, ambaye pia ni Mwenyekiti mkuu dunia wa chama hicho na mwanae Master Eiichi Miyazato, ambaye amewafanyia mitihani ya mkanda mweusi zaidi ya walimu 15 toka ngazi ya pili" Nidan" hadi ngazi ya saba "Nandan". 
  Kwa mujibu wa Sensei Rumadha, ngazi hizo zote kwa utamaduni wa mtindo wa Okinawa Goju Ryu Karate huchukua miaka mingi sana kupandishwa ngazi  tofauti na mitindo mingine. 
   Sensei Rumadha Fundi akiwafanyisha mazoezi wanafunzi saba hao kabla ya kuanza kufanya mtihani wao wa kupanda daraja katika Dojo la Hekalu la Kujilinda lililomo katika ukumbi wa Shule ya Msingi ya Zanaki jijini Dar es salaam Jumatatu usiku Januari 22, 2018
  Viongozi wakuu wa  Dojo la Hekalu la Kujilinda lililomo katika ukumbi wa Shule ya Msingi ya Zanaki jijini Dar es salaam  wakishuhudia  wanafunzi saba wakifanya mazoezi kabla ya mtihani Jumatatu usiku Januari 22, 2018. Kutoka kulia ni Sensei Wilfred Malekia, Sensei Mohamed Murudker na Sensei Rashid Almasi
    Sensei Rumadha Fundi akiendelea kuwafanyisha  mazoezi wanafunzi saba hao kabla ya kuanza kufanya mtihani wao wa kupanda daraja katika Dojo la Hekalu la Kujilinda lililomo katika ukumbi wa Shule ya Msingi ya Zanaki jijini Dar es salaam Jumatatu usiku Januari 22, 2018
  Sensei Rumadha Fundi akiendelea kuwafanyisha  mazoezi kwa vitendowanafunzi saba hao kabla ya kuanza kufanya mtihani wao wa kupanda daraja katika Dojo la Hekalu la Kujilinda lililomo katika ukumbi wa Shule ya Msingi ya Zanaki jijini Dar es salaam Jumatatu usiku Januari 22, 2018
   Sensei Rumadha Fundi akitoa mwongozo akiwa na uongozi wa dojo kabla ya  mtihani  wa kupanda daraja wa wanafunzi saba  katika Dojo la Hekalu la Kujilinda lililomo katika ukumbi wa Shule ya Msingi ya Zanaki jijini Dar es salaam Jumatatu usiku Januari 22, 2018
   Kutoka kushoto Ma-Senpai Abdulmajid Khan wa Hekalu la Kujilinda pamoja na  Shaaban Yusuf na Galant Swai ambao wanatoka katika tawi la Hekalu la Kujilinda lililopo mjini Dodoma kwa jina la Miyagi dojo wakifuatiwa na ma-Senpai Yusuf Kimvuli wa Kaizen dojo na Senpai Seif Soud wa Hekalu la Kujilinda.
  Wanafunzi watatu waliofaulu na kupanda daraja la kwanza (1st Dan) ama "Shodan" kutoka mkanda wa kahawia ni  kutoka kushoto ma-Senpai Abdulmajid Khan wa Hekalu la Kujilinda pamoja na  Shaaban Yusuf na Galant Swai ambao wanatoka katika tawi la Hekalu la Kujilinda lililopo mjini Dodoma kwa jina la Miyagi dojo.

  0 0


  Wafanyabiashara wakubwa wa mbolea Mkoani Rukwa pamoja na wakulima wameridhishwa na upatikanaji wa mbolea na kusifu juhudi za serikali baada ya kupaza sauti zao na kusikika na Rais Dk. John Pombe Magufuli na jambo hilo kufanyiwa kazi ndani ya muda mfupi.

  Wafanyabiashara hao wamesema kuwa wakulima hivi sasa hawapangi tena foleni kusubiri mbolea iliyokuwa ikipatikana kwa taabu na kwa kunyang’anyiana na kuwa foleni hizo zimekwisha na wakulima hawana haja ya kutoka Kijiji kuja mjini kufuata mbolea kwani mbolea hizo zinawafuata huko waliko hasa baada ya marekebisho ya bei elekezi iliyotolewa na Uongozi wa mkoa wa Rukwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

  Mmoja wa Wafanyabiashara hao wakubwa Mohamed Rashid Mdangwa wa Kampuni ya ETG amesema “Sasa wakulima wameanza kupata mbolea kwa wingi, mwanzo walikuwa wanapanga foleni hapa lakini kuanzia ile Jumatatu agizo la Rais kuwa mbolea iende Mkoa wa Rukwa, sasa hivi population (wingi) ya watu imepungua sana, sasa hivi mahitaji ya mbolea sio makubwa sana kama miezi miwili iliyopita,na mbolea ipo nyingi njiani inakuja, na bei elekezi aliyoitoa Mkuu wa Mkoa imesaidia mbolea kufika vijijini kupitia wakala wadogo wa mbolea.”

  Yamewsemwa hayo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kupitia maghala makubwa ya mbolea yaliyopo Sumbawanga Mjini pamoja na baadhi ya wasambazaji wadogo ili kujionea upatikanaji wa mbolea hizo tangu kutolewa kwa agizo la Rais Dk. John Pombe Magufuli la kusambaza mbolea hizo katika Mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini tarehe 8.1.2018.

  Mh. Wangabo aliwasihi wasambazaji wadogo wa mbolea kuendelea kujitokeza na kununua mbolea hiyo ambayo bei iliyopo sasa imezingatia maoni yao na haiumizi, hivyo kufanya hima kuhakikisha kuwa mkulima hakosi mbolea ili kuweza kubaki katika lengo la kuzalisha chakula kwa wingi na kuleta ushindani na mikoa mingine inayozalisha chakula.

  “Mimi nitoe wito tu kwa wale Agrodealers (wasambazaji wadogo wa mbolea) wafike kuendelea kununua mbolea, hata bei tumekwishazifikiria tena upya, kila Halmashauri katika Wilaya wamekwisha kaa na kutoa mapendekezo yao halisi ya kiusafirishaji, kwahiyo wafike wanunue mbolea na kutakuwa na faida, bei imezingatia hadi miundombinu iliyoharibika hakutakuwa na usumbufu,” Mh. Wangabo alifafanua.

  Mh. Wangabo alitembelea maghala matatu ya wafanyabiashara wakubwa waliopo mjini sumbawanga, TFC pamoja na maduka ya wasambazaji wadogo matatu na kuongea na baadhi ya wakulima ili kujithibitishia upatikanaji wa mbolea hiyo kwa maeneo ya mjini na inayopelekwa vijijini.

  Kwa msimu wa 2016/2017 Mkoa wa Rukwa ulilima Hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602. Kwa msimu huu wa Kilimo wa 2017/18 Mkoa umelenga kulima jumla ya eneo la Hekta 554,310.6 na kuvuna tani 1,669,746.2 za mazao ya chakula.
  Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, Kamanda wa Zimamoto Mkoani Rukwa akikagua mbolea katika ghala la Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) lililopo Sumbawanga Mjini. ​
  Mmoja wa Wasambazaji wakubwa wa mbolea Mkoa wa Rukwa Mohamed Mdanga (Kulia) akitoa maelezo ya upatikanaji wa mbolea Mkoani humo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo(kushoto) alipokwenda kumtembelea kwenye ghala lake na kukuta mbolea zai ya tani 300.
  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele wa kwanza kushoto)alipokuwa akipita mtaa kwa mtaa katika mji wa Sumbawanga kujionea biashara ya mbolea inavyokwenda katika maduka ya mbolea (hayapo pichani) huku akiwa ameambatana na Meya wa manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa (koti la Draft).
  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili kutoka kulia) akiwa amesimama mbele ya duka la mbolea kuulizia upatikanaji wa bidhaa hiyo katikati ya mji wa sumbawanga, Mkoani Rukwa.
  Timu ya wataalamu wa Kilimo, Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na Viongozi wa Manispaa ya Sumbawanga, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kupita duka hadi duka kujionea upatikanaji wa mbolea katika mkoa wa Rukwa.

  0 0

  Power on Fitness Gym iliyopo Mwenge, Kinondoni Jijini Dar es salaam imeandaa siku maalumu kwa ajili ya kujumuika pamoja, kufanya mazoezi na kuukaribisha mwaka mpya wa 2018.

   Shughuli hiyo itafanyika siku ya Jumamosi January 27, 2018  katika viwanja vya Posta vilivyopo Sayansi,  Kijitonyama. Shughuli hii itanzaa saa 12 asubuhi mpaka usiku.
  Siku hiyo kutakuwa na mazoezi ya kukimbia(Jogging) ambayo itaanza alfajiri ya saa 12, na kufuatiwa na mazoezi ya Aerobics, Steps, Zumba, Mpira wa miguu, na michezo mingine kama kuvuta Kamba, Kukimbiza Kuku nk.

  Baada ya mazoezi, kutakuwa na burudani kabambe ya muziki itakayoongozwa na bendi ya Skylight bila kusahau burudani ya muziki itakayoporomoshwa na Ma DJ wakali wa hapa nchini.
  Siku hiyo pia kutakuwa na Nyama choma itakayoandaliwa kiufundi na wapishi waliobobea, Supu bila kusahau vinywaji vya kila aina. 

  Wadahamini wa shughuli hiyo ni Kampuni ya JSP Marketing Link Limited ikishirikiana na Msouth Company, Dagaa Microfinance Limited, Simba Makini Group, Jaina Ice Cubes, Micgen Insurance Brokers, TTCL na wenyeji Power on Fitness Gym.

  0 0

  Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi leo (jana) amekutana na kufanya Mazungumzo na Viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari Kanda ya Kati Mjini Dodoma.

  0 0

  Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye kushoto akimkaribisha Kaimu Mkuu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela kulia alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam mapema jana tarehe 23/01/2018.
  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela akiweka sahihi katika kitabu cha wageni alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dar es Salaam, wakati alipofanya ziara yake mapema jana  tarehe 23/01/2018.
  Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye (aliyeketi mbele) pamoja na Viongozi Waandamizi wa Jeshi hilo wakimfuatilia kwa karibu, Kaimu Mkurugenzi MKuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela, wakati wa mazungumzo yao alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dar es Salaam mapema jana tarehe 23/01/2018.
  Picha ya Pamoja, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye (wa pili kushoto) akiwa na Viongozi Waandamizi wa Jeshi pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Richard Mayongela (wa tatu kulia), mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo, Jijini Dar es Salaam mapema jana tarehe 23/01/2018.Picha na Jeshi la Zimamoto Na Uokoaji

  IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA – JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

  0 0

  Na Mwamvua Mwinyi,Kisarawe

  VYOMBO vya ulinzi na usalama,Mkoani Pwani vimetakiwa kuwatafuta baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa ni vigogo,; kuvamia msitu wa Hifadhi wa Kazimzumbwi uliopo wilayani Kisarawe na kugawa viwanja.

  Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ,alitoa rai hiyo wakati alipotembelea msitu huo kujionea baadhi ya maeneo ambayo yalivamiwa na wavamizi hao.Alisema vigogo hao wamesababisha msitu huo kuingiliwa na kuvamiwa mara nne na kundi la watu ambao wanadai sehemu ya msitu ni mali yao. 

  Mhandisi Ndikilo ,alieleza kundi hilo limekuwa likiisumbua serikali kwa kwenda mahakamani na kushindwa .Aidha alisema vyombo hivyo vifanye ufuatiliaji kujua ni vigogo gani ambao wamekuwa wakiwatumia baadhi ya watu kwenda kushtaki mahakamani ili wapewe maeneo hayo kwa ajili ya viwanja .

  “Inadaiwa kuna kampuni ilikata viwanja zaidi ya 300 na kuwauzia watu jambo ambalo haliwezekani kwani msitu huo umehifadhiwa kisheria”alisema mhandisi Ndikilo.Mhandisi Ndikilo,alisema kuwa msitu huo ulindwe kwani ni kama mapafu ya kupumulia viwanda na hewa ukaa hivyo endapo msitu huo utaharibiwa itahatarisha afya za watu. 

  “Serikali ya mkoa haikibali hili,nimeshangazwa na kusikia kuna tume imekuja hapa Kisarawe na kuwahoji wataalamu mbalimbali juu ya suala la msitu huu wakati hakuna rufaa ya kesi ambayo ilifunguliwa na wavamizi ambao walishindwa”:;

  ” Wakae wakijua tume hiyo mimi siitambui wala mkuu wa wilaya haitambui sababu haijatoa taarifa,” alisisitiza mhandisi Ndikilo.Mkuu huyo wa Mkoa alisema inawezekana kuna vigogo wanaofanya mipango hiyo ili waweze kupewa eneo hilo kwa ajili ya maslahi binafsi. 

  Nae mkuu wa wilaya ya Kisarawe Happiness Seneda alisema, wavamizi hao wamekuwa wakiwatishia watakwenda kwa waziri mkuu hata kwa Rais Dk .John Magufuli kueleza wanaondolewa kwenye maeneo yao.

  Awali akielezea juu ya uvamizi wa msitu huo kaimu meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilayani Kisarawe,Endrew Mwenuo alisema wavamizi hao wamefanya uharibifu mkubwa kwa kukata miti kwa ajili ya mbao, kuchoma mkaa na ukataji wa miti kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

  Alieleza,wamekuwa wakifanya doria mara kwa mara lakini wavamizi hao wamekuwa wakiwatishia mgambo wanaofanya doria kwenye msitu huo.Mwenuo alisema,kumevunjwa vibanda na kuondolewa alama zilizowekwa na TFS ili kuondoa ushahidi wa eneo la msitu. 

  Msitu wa Kazimzumbwi,una ukubwa wa hekta 4,862 ulitangazwa kuwa msitu wa hifadhi 1954.
  Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo (Wa kwanza kushoto)na kaimu meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS)wilayani Kisarawe Mkoani Pwani, Endrew Mwenuo (wa pili kulia)na mkuu wa wilaya ya Kisarawe Happiness Seneda ( Wa kwanza kulia) wakiangalia namna uvamizi ulivyofanywa na baadhi ya watu na vigogo katika msitu wa Kazimzumbwi wilayani Kisarawe.
  Kaimu meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS)wilayani Kisarawe Mkoani Pwani, Endrew Mwenuo (kushoto) akimwelekeza jambo mkuu wa Mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo kuhusiana na uvamizi uliofanywa na baadhi ya watu na vigogo katika msitu wa Kazimzumbwi.Picha na Mwamvua Mwinyi

  0 0

   RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa na mazungumzo na Mfalme wa Dubai Shaikh Mohammed Bin Rashid Al Maktoum, Vice President, Prime Minister and Ruler of Dubai, alipofika katika makaazi ya Mfalme huyo Nchini Dubai akiendelea na ziara yake ya kiserikali katika Nchi za Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu (UAE ).
   RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali. Mohamed Shein, Mfalme wa Dubai Shaikh Mohammed Bin Rashid Al Maktoum, Vice President, Prime Minister and Ruler of Dubai, wakibadilisha mawazo na CEO na Rais Shirika la Ndege la Emirates Airline Sheikh.Ahmed Bin Saeed Al Makhtoum,baada ya mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa makaazi ya Mfame Nchini Dubai.
   RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiagana na Mfalme Shaikh. Mohammed Bin Rashid Al Maktoum, Vice President, Prime Minister and Ruler of Dubai, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika makaazi ya Mfalme Dubai akiwa katika ziara yake katika Nchi za UAE.   RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa na Ujumbe wake akizungumza na Wafanyabiasha wa Umoja wa Nchini za Falme za Kiarabu UAE (Business Community Chamber of Commerce Dubai) mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa jengo la jumuiya hiyo Dubai. Kwa habari zaidi BOFYA HAPA


  0 0

  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wavuvi wanaozunguka ziwa Rukwa kuhakikisha wanatafuta ardhi kwaajili ya kilimo, biashara pamoja na ufugaji katika kipindi cha kunzia mwezi wa kwanza hadi wanne kila mwaka ili kuwaacha samaki wa ziwa hilo kuzaliana.

  Amewaasa kutotegemea shughuli moja tu kwaajili ya kuwaingizia kipato, “Wavuvi msitegemee kuvua tu, jishughulisheni na kazi nyingine za kuwaingizia kipato kama vile kilimo, biashara pamoja na ufugaji, hatufungi kambi hizi kwaajili ya kipindupindu tu lakini pia ili kuweza kuwaacha samaki wazaliane katika kipindi cha kuanzia mwezi wa kwanza hadi wanne,”

  Ameyasema hayo alipofanya ziara kwenye kambi ya Nankanga iliyopo katika Kijiji cha Solola Wilayani Sumbawanga ili kujionea hali halisi ya maisha ya wavuvi katika kambi zisizo rasmi na namna ya kuweka mpango salama wa kuweza kuwaepusha na ugonjwa wa kipindupindu ulioenea katika makambi hayo yanayozunguka ziwa Rukwa. 

  Tangu ugonjwa huo uingie Mkoani Rukwa tarehe 15/11/2017 tayari watu 210 wanaugua ugonjwa huo na watu nane wamepoteza maisha wote wakiwa wanatokea katika makambi hayo yasiyo rasmi ambapo hadi sasa kambi zisizo rasmi zaidi ya tisa zimefungwa huku zoezi hilo likitegemewa kuendelea hadi hapo Mwezi wa tano.

  Nae Diwani wa kata ya Nankanga kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule amesema kuwa katika kambi hiyo kuna watoto 270 walio na umri chini ya miaka 7 ambao wamekosa kwenda shule na hivyo wananchi kujenga madarasa mawili ya shule shikizi katika kitongoji kilichopo Km 9 kutoka kwenye kambi hiyo yaliyofikia usawa wa linta na kumuomba Mkuu wa Mkoa kuwaunga Mkono jambo lililompelekea Mh. Wangabo kutoa bati 50 na kuitaka Halmashauri kuongezea bati 50 ili kukamilisha ujenzi huo.
  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwaasa wavuvi wa kambi ya Nankanga kujishughulisha na kilimo hasa katika kipindi cha mwezi wa kwanza hadi wa Nne kila mwaka pindi shughuli za uvuvi zinapofungwa ili kuwaacha samaki wazaliane na kutunza Ziwa lisipotee kwa faida ya vizazi vijavyo.

  0 0

   
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) pamoja na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kulia) wakizungumza na Mbunge wa viti maalumu, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Zainabu Mwamwindi wakiwa wameongozana na Wajumbe Kamati hiyo wakati walipotembelea jana Jengo la Makumbusho ya Olduvai ya Gorge ambako ni chimbuko la historia ya Binadamu katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
  Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kulia) akizungumza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) wakiwa na Wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakati walipotembelea jana Jengo la makumbusho ya Olduvai ya Gorge ambako ni chimbuko la historia ya Binadamu katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro

  Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii , Kemilembe Luota ( wa kwanza kushoto) Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) pamoja na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudence Milanzi (wa pili kulia) wakiwa na baadhi ya Wajumbe wa kamati hiyo wakiwa kwenye ‘’View Point’ kituo ambacho hutumika kuangalia bonde la Ngorongoro kabla ya kutelemka katika Bonde hilo jana wakati walipofanya ziara ya kutembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
  Huyu ndiye Faru Fausta ni faru kikongwe kuliko wote nchini, akiwa na umri wa miaka 54, na anahitaji matunzo mazuri ili aendelee kuvuta watalii na wanasayansi kutoka kila pembe ya dunia.

  Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Waandishi wa habari wakiji’selfie’ katika banda la Faru Fausta ambaye ndiye faru kikongwe kuliko wote nchini, akiwa na umri wa miaka 54, na anahitaji matunzo mazuri ili aendelee kuvuta watalii na wanasayansi kutoka kila pembe ya dunia wakati walipotembelea banda hilo kwa ajili ya kujionea
  Baadhi ya Msururu wa Magari yaliyokuwa yamewbeba wjumbe wa kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na viongozi na watumishi wa Wizara pamoja na wa Ngorongoro kwa ajili ya kutelemka kwenyeBonde la Ngorongoro.
  Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiwa katika nje ya ofisi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kuanza ziara.
  Kundi la Simba wakiwa wamepumzika walipoonekana jana wakati Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipofanya ziara ya kutembelea Bonde la Ngorongoro.
  Bonde la Olduvai Gorge ambako ni chimbuko la historia ya binadamu ni kivutio cha kinachowavuta watalii wengi kutembelea eneo hilo.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga( wa kwanza kushoto) akiteta jambo na Wakurugenzi wa Wizara hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea jana Makumbusho ya Olduvai GorgeMhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Freddy Manongi akizungumza jana kwenye kikao cha Majumuisho na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii mara baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea Bonde la Ngorongoro na Makumbusho ya Olduvai Gorge.(PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA –MALIASILI NA UTALII  Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kazi nzuri iliyofanya ya ujenzi wa jengo la makumbusho ya kisasa katika Bonde la Olduvai ya Gorge ambako ni chimbuko la historia ya Binadamu.

  Kamati hiyo imesema imeridhishwa na ujenzi wa jengo hilo ambalo litawavutia watalii na wanasayansi wabobezi wa masuala ya Malikale kutembelea Makumbusho hiyo.

  Kamati hiyo ilibainisha kuwa Makumbusho hiyo mbali ya kutumika kuingiza pesa kupitia watalii pia inatumika kama kielelezo na utambulisho muhimu wa taifa katika kutangaza utamaduni wa Mtanzania ndani na nje ya nchi.

  Hayo yalisemwa jana na Kamati hiyo wakati ilipofanya ziara ya kutembelea Ngorongoro Crater na Makumbusho ya Olduvai Gorge katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

  Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Kemilembe Luota ameipongeza Serikali pamoja na wataalamu kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuhakikisha kuwa eneo la Olduvai Gorge linakuwa kivutio bora kwa ajili ya historia ya nchi na kivutio kikubwa cha Utalii duniani.

  ‘’ Sisi kama Kamati tunaipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuyafanyia kazi mapendekezo yote tuliyoyatoa kwa mara ya kwanza tulipokuja kwa vile tumeona kazi nzuri imefanyika.’’

  Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi kutembelea makumbusho hiyo kwa vile idadi ya watalii wa ndani aliyokutana nayo sio ya kuridhisha.

  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema makumbusho hiyo inatoa ushahidi dhahiri kuwa hata wazungu, mababu zao walitoka Afrika.

  Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema Makumbusho hiyo hadi hapo ilipofikia imeboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu hata hivyo ameitaka Wizara ihakikishe inaitangaza ipasavyo ili watalii wengi zaidi wazidi kutembelea.

  Awali, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, FredyManongi amesema tangu kuzinduliwa kwa makumbusho hiyo kwa wiki moja imekuwa ikipokea zaidi ya watalii wapatao 40000 hali inayopekelea kuwa ni miongoni mwa Makumbusho inayofanya vizuri zaidi barani Afrika

  0 0

  Naibu Waziri OR-TAMISEMI Mhe Josephat Kandege akimskiliza Meneja wa TBA Mkoa wa Mara wakati alipotembelea eneo ya ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Butiama
  Hapa ndipo mradi ulipofikia wa ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama inayojengwa na TBA ambao mkataba wake umesitishwa
  Hii ndio Kazi iliyofanyika mpaka sasa kwenye eneo la Ujenzi ilihali taarifa iliyotokewa kwa Waziri Mkuu ni kuwa ujenzi wa Msingi umefikia asilimia 60

  Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Josephat Kandege ameagiza kuvunjwa kwa Mkataba wa Tsh Bil 3.2 kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama iliyokuwa ikijengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

  Mhe Kandege ameyasema hayo kufuatia Ukaguzi aliyoufanya baada ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa aliyekamilisha ziara yake Mkoani hapa kumuagiza kufanya Ukaguzi huo kutokana na kutoridhishwa na taarifa aliyoipokea kutoka kwa Meneja wa TBA Mkoa wa Mara kuhusiana na mradi huo.

  Mhe Kandege alisema kuwa katika ukaguzi wake amebaini kuwepo kwa kasi ndogo ya utekelezaji wa Mradi huo na kubadilishwa kwa eneo lililofanyiwa usanifu hapo awali kwa ajili ya ujenzi badala yake kazi hiyo kufanyika katika eneo tofauti na lile la awali hivyo kuiongezea Serikali gharama ya Tsh Mil. 180.

  Aidha, aliongeza kuwa taarifa iliyotolewa na Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Mara kwa Waziri Mkuu ilieleza kuwa kati ya Tsh. mil. 600 zilizopokelewa Aprili, 2017 kutoka Serikali kuu, Tsh Mil. 400 zimekwishatumika kujenga msingi na kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 60 tofauti na hali aliyoikuta alipotembelea eneo hilo la Mradi.

  Alisema ‘Nimeshangazwa kuona hakuna msingi wowote uliojengwa mpaka sasa katika eneo la Mradi kwa hali hii Mtendaji huyu wa TBA ametoa taarifa ya uongo kwa Mhe. Waziri Mkuu’

  ‘Kwa kuzingatia makosa hayo yote Serikali inaagiza kuvunjwa kwa Mkataba wa ujenzi wa Ofisi za Halmashauri uliokuwa utekelezwe na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushindwa kutekeleza mradi huu kwa wakati, kuongeza gharama za mradi kinyume cha taratibu bila kupata kibali cha Baraza la Madiwani na Ofisi ya Rais TAMISEMI sambamba na kutoa taarifa za uongo kwa Mhe. Waziri Mkuu. Aliongeza Mhe. Kandege.

  Kwa Mujibu wa Taarifa ya Mhe Kandege Kandarasi hiyo imesitishwa hadi hapo Serikali itakapotoa maelekezo mengineyo.Mhe Kandege aliambata na Waziri Mkuu katika ziara hiyo iliyodumu kwa muda wa siku saba mkoani Mara na mpaka sasa bado anaendelea na ufuatiliaji wa maagizo mbalimbali aliyopewa na Mhe. Waziri Mkuu wakati wa ziara hiyo mkoani hapo.

  0 0

  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa miezi mitatu kwa wananchi wanaoishi katika kambi ya uvuvi ya Nankanga iliyopo kando ya ziwa Rukwa kuhama kwa hiyari baada ya kambi hiyo kuwa katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kipindupindu kwa kutokuwa na vyoo.

  Mh. Wangabo amesema kuwa kuondoka huko kwa hiari kuwepo ndani ya mwezi huu wa kwanza hadi wa nne baada ya kuona wingi wa wananchi wanaoishi katika kambi hiyo pamoja na kutokuwepo kwa kipindupindu kwa wakati huu ila zoezi hilo ni la tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huo.

  “Hatuwezi kuendelea kuishi mahali hapa ambapo vyoo vyenyewe vinaingiliana na maji ya kunywa, na ili kisije hapa kipindupindu ni lazima watu wasifanye shughuli kwenye ziwa ili kuwe salama, lakini mkiruhusu kipindupindu kuingia hapa tutawafurusha, tena tutawasimamia kweli kweli, tutawapiga quarantine (kuwaweka kwenye kizuizi) mkipona tutawaswaga,” Amesisitiza

  Ameyasema hayo alipofanya ziara kwenye kambi ya Nankanga iliyopo katika Kijiji cha Solola Wilayani Sumbawanga ili kujionea hali halisi ya maisha ya wavuvi katika kambi zisizo rasmi na namna ya kuweka mpango salama wa kuweza kuwaepusha na ugonjwa wa kipindupindu ulioenea katika makambi hayo yanayozunguka ziwa Rukwa. 

  Nae Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule alitoa hadi tarehe 1/5/2018 wananchi hao wawe wameyahama makazi hayo na kujisogeza kwenye vitongoji vya jirani huku akiwasihi viongozi wa vijiji na vitongoji hivyo kushirikiana kuhakikisha wanatoa maeneo kwaajili ya wananchi hao kuhamia.

  “Kuanzia tarehe 1 mwezi wa 5 hapa hatutaki kumuona mtu, kama una kibanda chako ama bati lako anza sasa hivi kwa kushirikiana na mwenyekiti wa Kijiji na Mtendaji wa Kata mtafute nafasi katika kitongoji cha Isanga kila mtu ajenge nyumba,” Alisisitiza.

  Hatua hiyo imekuja baada ya ugonjwa wa kipindupindu kusambaa kwenye kambi kadhaa za wavuvi pembezoni mwa ziwa rukwa na kusababisha watu 210 kuumwa ugonjwa huo na watu nane kupoteza maisha, ambapo hadi sasa kambi zisizo rasmi zaidi ya tisa zimefungwa huku zoezi hilo likitegemewa kuendelea hadi hapo Mwezi wa tano.
   Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa kwanza mbele kulia) akiwa ameambatana na mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule wakitembelea kambi ya mererani waliyohamishwa wavuvi kwa nguvu ili kuepuka kipindupindu na kulinda mazingira ya ziwa hilo. 
   Moja ya kibanda kilichokuwa katika kambi ya Wavuvi ya Mererani kikiwaka moto ikiwa ni juhudi za kuwaondoa wavuvi waliopo ndani ya Ziwa Rukwa kuwaepusha na kipindupindu na kulinda ziwa lisipotee. 
   Miongoni mwa wananchi waliokuwa wakiishi katika makambi ya wavuvi yalipo ndani ya Ziwa Rukwa yaliyoathiriwa na kipindupindu wakisimamiwa kuhama kambi hiyo ili kujiepusha na kipindupindu na kuliza Ziwa.
   Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa tahadhari kwa Wavuvi waliohamishwa kwenye makambi (hawapo pichani) kutorudi katika makambi hayo kwa usalama wa afya zao na kuendelea kulitunza ziwa Rukwa. 
   Miongoni mwa Vyoo vinavyotumiwa na Wavuvi wa kambi ya Nankanga waliopewa miezi mitatu kuihama kambi hiyo kabla ya kipindupindu kuwamaliza. 
  Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipoongozana na kamati ya ulinzi na Usalama kuangalia moja ya choo kinachotumiwa na wavuvi wa kambi ya Nankanga, choo ambacho si salama kwa matumizi ya binadamu.

  0 0

  Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha Umeme wa msongo wa kV 33 inayojengwa kuelekea eneo litakalotumika kuzalisha Umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

  Dkt. Kalemani aliyasema hayo mkoani Morogoro wakati alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa kazi ya maandalizi ya ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 2100 pamoja na kuzungumza na wananchi katika vijiji vinavyopitiwa na miundombinu hiyo ya kusafirisha Umeme.

  Dkt. Kalemani alisema kuwa, maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa Umeme wa Stiegler’s yanajumuisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya Barabara na usafirishaji Umeme kuelekea eneo la Mradi ili mradi huo mkubwa utekelezwe kwa ufanisi. 

  Alieleza kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo ya usafirishaji umeme unatekelezwa na kampuni ya ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO na kwamba miundombinu hiyo inajengwa kutoka katika kituo cha kituo cha kupoza umeme cha Msavu hadi Mto Rufiji ambapo ni takriban kilometa 170.

  “Kwa Vijiji ambavyo vinapitiwa na mradi huu wa njia ya kusafirisha umeme, wananchi watafungiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kama ilivyo katika vijiji vingine vinavyopitiwa na miradi ya usambazaji umeme vijijini na hakuna fidia kwa wananchi watakaopisha miundombinu hii,” alisema Dkt Kalemani.

  Alisema kuwa, mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Februari mwaka huu mara baada ya Mkandarasi kupatikana na kwamba ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kuelekea eneo hilo la mradi umetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 80 na utakamilika mwezi Aprili mwaka huu.

  Meneja Mradi wa Stiegler’s Gorge kutoka TANESCO, Florence Gwang’ombe, alisema kuwa mradi huo wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme utaboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo ambayo hayakuwa na Umeme ikiwemo baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Morogoro, vijiji vya Matombo, Dakawa, Kisaki pamoja na kambi ya Maafisa wa Wanyamapori ya Matambwe.

  Alisema kuwa, mradi unatarajiwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 6.1 hadi kukamilika kwake na kwamba nguzo zinazotumika katika mradi huo ni za miti na zege na katika sehemu nyingine umeme utasafirishwa kwa kutumia nyaya zitakazopitishwa ardhini.

  Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alimpongeza Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya uamuzi wa kuanza kutekeleza mradi huo wa Stieglers Gorge ambao alisema kuwa utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini, utainua uchumi wa nchi kutokana na kuchochea uanzishwaji wa viwanda pamoja na maendeleo ya mtu mmoja mmoja kupitia shughuli mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme.
   Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( wa Nne kushoto) akikagua maeneo ambayo miundombinu ya usafirishaji umeme inajengwa kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100. Wa Tatu kulia ni Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo na wengine ni watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO.
   Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO wakati alipokuwa katika kijiji cha Dakawa mkoani Morogoro kukagua miundombinu ya usafirishaji umeme inayojengwa kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100.
  Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100 ikiendelea. Kazi hiyo inatekelezwa na  kampuni ya  ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO.

  0 0

  Kampuni ya uchunguzi na utafiti wa madini, Helium One, ambayo kwa sasa inafanya utafiti wa gesi ya heliamu mkoa wa Rukwa imegundua kuwapo kwa futi za ujazo bilioni 98.9 za gesi hiyo katika maeneo iliyokwishafanyia uchunguzi. 

  Hayo yalielezwa katika warsha ya siku moja iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na kuratibiwa na Idara ya Jiolojia ya chuo hicho, Helium One na Chuo Kikuu cha Oxford.

  Akizungumza katika warsha hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Helium One, Thomas Abraham-James, alisema kwamba kampuni yao imetafuta leseni 23 za uchunguzi na kwamba nyingine tatu zimeombwa.

  Alisema kwamba leseni hizo zote zinamilikiwa na kampuni hiyo kwa asilimia 100 na kwamba ina haki za kipekee za gesi hiyo ya heliamu .

  Pamoja na kutoa taarifa hiyo,alisema lengo la kuwa na warsha ni kuwaita wataalamu na wadau mbalimbali wa hapa nchini na kimataifa kubadilishana uzoefu na taarifa zilizopo kuhusu gesi hiyo na kuangalia fursa zinazoambatana na uwapo wa gesi hiyo katika harakati za kitaifa za kuwa na taifa la viwanda.

  “Helium One inaamini kwamba kuna fursa kupitia utafiti huu kuweza kutengeneza utaalamu wa kiwango cha juu na utaalamu wa hapa nchini juu ya uendelezaji wa gesi hiyo. Tutaendelea kujenga uhusiano na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuweza kubadilishana elimu, kutoa mafunzo kwa wanafunzi na maofisa wizara ya madini na kutengeneza mpango wa ufadhili wa masomo,” alisema.

  Kwa mujibu wa Abraham-James, warsha hiyo ilihudhuriwa na wanasayansi waandamizi wa gesi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza na Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam,UDSM, watu wenye mamlaka na maamuzi, wadau wa maendeleo, watengeneza sera kutoka serikalini, watafiti na sekta binafsi.

  Aidha kampuni hiyo imetoa ufadhili wa masomo ngazi ya shahada ya uzamili kwa wanafunzi wawili wa UDSM kusoma katika Chuo Kikuu cha Oxford , ikiwa ni sehemu ya kuingiza utaalamu wa hali ya juu wa kisayansi kwa watanzania na pia kuendeleza uhusiano mzuri kati ya Helium One na UDSM.

  Wakati wa warsha hiyo, Profesa John Machiwa, akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, Prof Cuthbert Kimambo, alisema kwamba jukwaa hilo ni jema kwa wanafunzi, wakufunzi na Chuo kizima kutafuta njia ya kuona namna ya kushirikiana na Helium One.

  “Tunaweza kufanyakazi pamoja na kunoa taaluma na pia kupata utaalamu katika utafiti wa heliamu uzalishaji na usafirishaji wake,” alisema.
    Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya utafutajji gesi ya Helium One, Thomas Abraham-James, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati wa warsa juu ya ugunduzi wa gesi ya Helium iliyoandaliwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Hudson Nkotago akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana wakati wa warsa juu ya ugunduzi wa gesi ya Helium iliyoandaliwa na kampuni ya utafutaji wa gesi ya Helium One kwa kushirikiana na Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

  0 0


  0 0

  Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA

  Serikali imemshtaki John Hima (29) kwa kosa la kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Namba 9 ya mwaka 2015.

  Akisoma kesi hiyo namba 9 ya mwaka 2018 katika Mahakama ya Wilaya ya Bahi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Suniva Mwajumbe, Inspekta Msaidizi Amani amesema kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo Januari 7 mwaka huu katika kijiji cha Nghulukano, Kata ya Chikola, Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma.

  Ilielezwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa ni mwajiriwa wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akiwa ni mkusanya taarifa (mdadisi) katika Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa Mwaka 2017/2018 kwa Tanzania Bara.

  Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mdadisi Hima alikana mashitaka na kesi hiyo itasomwa tena tarehe 7 Februari, 2018 ambapo amerudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini.Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, Mwanasheria wa NBS Oscar Mangula amesema kuwa, mtuhumiwa Hima aliingia mkataba na NBS kuwa mmoja wa wadadisi wa Utafiti huo unaoendelea hivi sasa ambao ulianza Desemba mwaka jana.

  “Kwa mujibu wa sheria akiwa kama mdadisi majukumu yake alitakiwa kuwa katika eneo la kazi kulingana na mkataba na kiapo alichopata ambapo yeye kwa makusudi aliamua kutelekeza majukumu hayo na kuwa nje ya kituo cha kazi hivyo kwa mujibu wa sheria ya Takwimu ametenda kosa la kijinai” amesema Mwanasheria Mangula.

  Mwanasheria Mangula ameongeza kuwa, “Mkataba wa kazi ni wa miezi 12 ambapo ulianzia Desemba 2017 hadi Novemba 2018 lakini mdadisi huyu aliacha kutimiza majukumu yake kuanzia tarehe 7 Januari ambapo sisi tulifika pale tarehe 13 na 14 Januari mwaka huu ila hakuweza kufanya kazi yake kama ilivyotakiwa”.

  Mwanasheria Mangula alieleza kuwa kesi hiyo inawakumbusha wadadisi waliopewa jukumu la kukusanya taarifa za kitakwimu kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira, kiapo na mafunzo waliyopewa ili kuepuka kutenda makossa ya kijinai kama analodaiwa kutenda na mtuhumiwa.

  Aidha, inawakumbusha wananchi umuhimu wa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wadadisi mbalimbali wanaopewa jukumu la kukusanya taarifa za kitakwimu kwani kufanya hivyo ni kutekeleza matakwa ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

  0 0


  0 0

  Mwakilishi wa mshindi wa Tigo pesa wakala David Lucas,Joyce David(wa pili kushoto) akipokea mfano wa hundi kutoka kwa Mkurugenzi wa Tigo kanda ya Ziwa Joseph Mutalemwa(kulia), wakati wa hafla ya kuwapa zawadi mawakala waliofanya vizuri kwenye miamala ya Tigo pesa iliyofanyika jijini Mwanza jana, kushoto ni Mratibu wa Tigo wa Masoko na Biashara kanda ya Ziwa Abraham Mchau akishuhudia.


  Mwakilishi wa mshindi wa Tigo pesa wakala kutoka Kahama mkoani Shinyanga Asha Athuman,Daud Kilonzo akipokea mfano wa hundi kutoka kwa Mkurugenzi wa Tigo kanda ya Ziwa Joseph Mutalemwa(kushoto), wakati wa hafla ya kuwapa zawadi mawakala waliofanya vizuri kwenye miamala ya Tigo pesa iliyofanyika jijini Mwanza jana, kulia ni Meneja wa Tigo kanda ya Ziwa Kaskazini Daniel Mainoya akishuhudia

  Washindi wa Tigo pesa wakionyesha mfano wa hundi zao baada ya kukabidhiwa jijini Mwanza.  Mawakala na wateja wa mtandao wa Tigo wakishundua utoaji wa hundi kwa wateja wa tigo pesa jijini Mwanza.

  Mawakala na wateja wa mtandao wa Tigo wakishundua utoaji wa hundi kwa wateja wa tigo pesa jijini Mwanza.
  Mkurugenzi wa Kampuni ya Tigo-Tanzania Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga (kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi ya Sh1 milioni Wakala wa Tigo Pesa, Asha Ramadhani kutoka Mkoani Ruvuma baada ya kuibuka mshindi kwa kufanya vizuri kwenye huduma ya TigoPesa katika droo inayochezeshwa na kampuni hiyo.  Hafla hiyo ilifanyikia Makao Makuu ya Ofisi za Tigo Kanda hiyo zilizopo Uhindini Jijini Mbeya.
  Mkurugenzi wa Kampuni ya Tigo-Tanzania Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga (kutikati) akizungumzia zawadi zilizotolewa kwa washindi wa droo inayochezeshwa kwa mawakala wa Tigo Pesa, Yusuph Kigomba (kushoto) kutoka Mkoani Iringa na Asha Ramadhani kutoka mkoani Ruvuma ambao  waliibuka washindi kwa kufanya vizuri kwenye huduma ya TigoPesa.  Hafla hiyo ilifanyikia Makao Makuu ya Ofisi za Tigo Kanda hiyo zilizopo Uhindini Jijini Mbeya.

  0 0


  0 0

  Jaji Mstaafu Robert Kisanga enzi za uhai wake.


older | 1 | .... | 1496 | 1497 | (Page 1498) | 1499 | 1500 | .... | 1904 | newer