Quantcast
Are you the publisher? Claim or contact us about this channel


Embed this content in your HTML

Search

Report adult content:

click to rate:

Account: (login)

More Channels


Showcase


Channel CatalogChannel Description:

Karibuni Jamvini Wanajamii

older | 1 | .... | 1087 | 1088 | (Page 1089) | 1090 | 1091 | .... | 1897 | newer

  0 0


  Usiku wa 31,December 2016 kuamkia mwaka mpya 2017 ndipo wanamitindo mbalimbali walikutana na kusherekea kwa pamoja Usiku wa Khanga yaani “Khanga Party”. Tukio hili kama lilivyo kuwa limetaarifiwa awali limefanyika Regency  Park Hotel.  Design mbalimbali za vazi la Khanga kutoka kwa wanamitindo zilioneshwa kwenye stage na kuzikonga mioyo za wadau pamoja na wahudhuriaji  usiku huo.

  Kumbuka Party hii imeandaliwa na Mama wa Mtindo maarufu kama Asya Idarous Khamsin, mbali na burudani zilizo kuwepo pia kulikuwa na Red Carpet yenye sifa kubwa ya kuwakutanisha mastaa na mashabiki wao kuweza kupiga picha za pamoja kwa ajili ya kumbukumbu. Tunawatakia mwendelezo mwema na wenye baraka wadau na wanamitindo kutoka hapa Tanzania. (Cheers 2017)

  0 0


  0 0

   Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Funguo za Gari aina Mpya ya Noah  Mkuu wa Mkoa Mstaafu Mhe, Abdalla Mwinyi Khamis iliyotolewa na Ofisi ya  Mkoa Mjini Magharibi jana katika sherehe za Kumpongeza kwa Utumishi uliotukuka  katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,hafla iliyofanyika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazi Mmoja Mjini Unguj.
  mwimbi-1
  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akipena mkono na Mkuu wa Mkoa Mstaafu Mhe, Abdalla Mwinyi Khamis kama ishara ya kumkabidhi  Gari aina Mpya ya Noah iliyotolewa na Ofisi ya  Mkoa Mjini Magharibi  katika sherehe za Kumpongeza Mstaafu huyo kwa Utumishi wake katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,hafla iliyofanyika  jana katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazi Mmoja Mjini Unguja,[Picha na Ikulu.
  mwimbi-2
  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe,Ayoub Mohamed Mahmoud (kulia) wakiwa na  Mkuu wa Mkoa Mstaafu Mhe, Abdalla Mwinyi Khamis katika sherehe za Kumpongeza Mstaafu huyo na kumzawadia zawadi mbali mbali ikiwemo Gari aina ya Noah yenye thamani Millioni kumi na Mbili ,katika hafla iliyofanyika  jana katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazi Mmoja Mjini Unguja,[Picha na Ikulu.
  mwimbi-5
  Viongozi mbali mbali waliohudhuria katika hafla ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa Mjini Magharibi Mhe, Abdalla Mwinyi Khamis katika sherehe za Kumpongeza kwa Utumishi wake uliotukuka    na kumzawadia zawadi mbali mbali ikiwemo Gari aina ya Noah yenye thamani Millioni kumi na Mbili,katika hafla iliyofanyika  jana katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazi Mmoja Mjini Unguja,[Picha na Ikulu.
  mwimbi-3
  Baadhi ya Viongozi mbali mbali waliohudhuria katika hafla ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa Mjini Magharibi Mhe, Abdalla Mwinyi Khamis katika sherehe za Kumpongeza kwa Utumishi wa muda mrefu uliotukuka na kumzawadia zawadi mbali mbali ikiwemo Gari aina ya Noah yenye thamani Millioni kumi na Mbili,katika hafla iliyofanyika  jana katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazi Mmoja Mjini Unguja.
  mwimbi-4
   Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa Mjini Magharibi Mhe, Abdalla Mwinyi Khamis akipokea Taarifa ya pongezi zake kwa ushirikiano uliotukuka kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini Marina Joel Thomas baada ya kuisoma jana wakati wa sherehe maalum ya kumpongeza na kumzawadia,iliyofanywa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazi Mmoja,(katikati)Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo.
  mwimbi-6
   Mwimbaji wa Kikundi cha Zanzibar One Marium Juma akiimba wimbo wa “Nadekezwa” wakati wa sherehe ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa Mjini Magharibi Mhe, Abdalla Mwinyi Khamis zilizofanyika jana katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazi Mmoja,liyofanywa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi chini ya usimamizi wa Mhe,Ayoub Mohamed Mahmoud,[Picha na Ikulu.] 31/12/2016.

  0 0


  0 0

   Mbunge wa viti maalum mkoa waIringa(CCM) Rita Kabati akiongea na familia ya watu watano wenye ulemavu wa viungo alipowatembea katika kijiji cha Lulanzi kata ya Mtitu wilayani Kilolo mkoa wa Iringa wakati wa kuwasaidia msaada kukarabati nyumba yao pamoja na kuwapa vitu vingine vya kimsaada
  Leah mwamoto mtoto wa mbunge wa jimbo la kilolo Vennance Mwamoto naye alishuhudia maisha magumu wanaoishi familia ya watu watano wenye
  ulemavu wa viungo alipowatembea katika kijiji cha Lulanzi kata ya Mtitu wilayani Kilolo mkoa wa Iringa na hapo aliposimama ndio choo kinachotumiwa na familia hiyo kwa sasa huku wakisubili ujenzi wa choo kipya kinachoendelea kujengwa kwa hisani ya mbunge Ritta kabati
  Hivi ni baadhi ya vifaa vilivyoletwa na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Rita Kabati kwa ajili ya kuwasidia familia ya watu watano wenye ulemavu wa viungo alipowatembea katika kijiji cha Lulanzi kata ya Mtitu wilayani Kilolo mkoa wa Iringa

  Na fredy mgunda,Iringa

  FAMILIA ya watu watano wenye ulemavu wa viungo wamemuomba mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Rita Kabati kuendelea kuilea familia hiyo kama familia
  yake.

  Akizungumza na blog hii mmoja wa wanafamilia hiyo,Elias Mpogole ambaye ni mlemavu alisema kuwa mbunge huyo amekuwa akiwasaidia toka siku ya kwanza walipokutana naye katika kijiji hicho cha Lulanzi.

  “Zamani tulikuwa tunaishi kwenye nyumba ambayo inavuja haina dilisha wala mlango pia tulikuwa tunalala chini lakini mbunge Kabati katusaidia nyumba nzuri kama mnavyoiona waandishi,katuletea magodoro,mashuka,blanket na sasa ameanza kutujenga choo cha kisasa na ameshawalipa mafundi pesa zote ndio maana tunaomba anendelee kuwa na sisi.”Alisema Mpogole

  Mpogole alishukuru msaada waliopatiwa na kuwataka wadau wengine waweze kujitokeza zaidi kuwasaidia kuwapatia vyakula na radio za kuwezakusikiliza nyimbo za dini.

  Kwa upenda wake mbunge wa viti maalum mkoa waIringa(CCM) Rita Kabati ametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo ukarabati wanyumba kwa familia yenye watoto walemavu wanne wa kijiji cha Lulanzi kilichoko kata ya Mtitu wilayani Kilolo mkoa wa Iringa. 

  Msaada huo wa ukarabati wa nyumba,umeambatana na magodoro, vyakula na ujenzi wa choo cha kisasa ameutoa baada yakuwahidi kufanyia matengenezo ya nyumba ambayo walikuwa wakipata shida
  kipindicha masika mara baada ya kufanya ziara mapema mwaka huu katika kijiji hicho nakugundua mateso wanayokumbana nayo familia hiyo. 

  “Nimeitembelea familia hiinimeumia sana kwani maisha wanayoishi ni ya shida sana hawana msaada wowotenyumba yao inavuja hawana chakula maishayao ni ya kuunganga unga mpaka watu wajekama sisi kuwaletea vitu  vidogo vidogokama mchele na mafuta na mbaya Zaidi hata watoto hao wote watatu hakuna hatammoja aliyewahi kukanyaga shule ingawa
  wanaonekana ni wakubwa hivyo jamii tunapaswa kuwasaidia watoto hawa” alisema Kabati 

  Familia hiyo ambayo baba mzazi Mzee LucasMpogole mbaye kwa sasa amelazwa hospitali ya mkoa wa Iringa kwa ugonjwa wakupooza ina watoto wanne wote wakiwa walemavu wa viungo hivyo kukosa msaadakabisa pindi mvua zikianza kijiji hapo. 

  Akizungumza wakati wa kukabidhimsaada huo , Kabati alisema kuwa jamii ya walemavu wanahitaji msaada wa hali namali kutoka kwa wadau wenye uwezo na kuacha tabia ya kuiacha serikali peke yakekatika kutatua kero zao na kuwahudumia.

  Alisema kuwa msaada huo utawafarijiwalemavu hao waone kuwa pamoja na upungufu walionao bado jamii ya watanzaniainawathamini
  na kuwajali katika maisha yao ya kila siku.

  Aliongeza kuwa walemavu wanayo hakiya kuishi na kujitegemea iwapo jamii itawajengea uwezo badala ya kuwafungiandani na kuwaona kama ni mkosi katika familia ila kugundua vipajiwalivyonavyo na
  kuiwezesha serikali kuwaingiza katika mipango mbalimbali yakuwapatia huduma. 

  Kabati alitoa wito kwa serikalikuona umuhimu wa kutumia vituo mbalimbali vinavyolea watoto wenye ulemavukuhakikisha vinawejengea miundo mbinu rafiki na uboreshaji mipango na mfumo wautoaji elimu, afya na usafiri kulingana na tofauti za umri wa watoto nchini. Aidha Kabati alitoa
  wito kwa Mfukowa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuangalia kwa jicho la tatu familia ya Mpogolekwa kuwaongezea kipato zaidi cha kila mwezi kwani kwa hali waliyonayo nakiwango wanachopata kila baada ya miezi miwili hakiendani na uwingi wa walemavuwa familia hiyo maskini. 

  Naye baba mdogo wa watoto hao akiongea kwa niaba ya baba mzazi wa walemavu hao, Juma Mpogole alimshukurumbunge huyo kwa msaada aliotoa na kumtaka awasomeshe watoto wake ambao tangu wazaliwe
  hawajawahi pata elimu yoyote licha ya kufikisha umri wa miaka zaidi 20.

  Lakini naomba nitoe rai kwa wale wanasiasa na wananchi wengine wanaokuja kupiga picha nah ii familia ya watu wenye ulemavu wa viungo kwa ajili ya kujitafutia umaarufu waache tabia
  hiyo.

  “Kila mara tunaona waandishi na wapiga picha wanafika hapa na viongozi mbalimbali lakini kila siku wanatoa ahadi tu sioni msaada wowote ule unaotolewa zaidi ya kuona wanajitafutia umaarufu huko mitaani naomba waacha tabia hiyo sisi tunamuona mbunge Ritta Kabati na kaka yake mbunge wa jimbo hili la kilolo Vennence mwamoto ndio
  wanaosaidia familia hii,kweli familia hii inaitaji msaada hivyo njooni kutoa
  msaada sio kupiga picha pekee yake”.alisema Mpogole

  0 0

  Na Rhoda Ezekiel Kigoma,

  CHAMA Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kasulu Kimemuomba Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Magufuli kuitimiza ahadi yake ya kuwasaidia Wananchi wa Wilaya ya Kasulu ya Kutatua Migogoro ya Mipaka inayo endelea baina ya Wananchi na eneo la hifadhi ya Misitu ya kagerankanda kama alivyo wahahidi Wananchi hao Wakati wa Kampeni kutatua kero hiyo endapo watakichagua Chama hicho.

  Akizungumza na gazeti hili katibu mwenezi wa Wilaya ya Kasulu Masoud Kitowe alisema wakati wa kampeni Rais aliwaomba Wananchi hao wakichague Chama cha mapinduzi na kuwaahidi endapo watakichagua chama hicho atahakikisha anatatua mgogoro huo na kuongeza mipaka Kwa Wananchi hao waweze kulima,na Wananchi walikichagua chama hicho mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.

  Alisema CCM Wilaya ya Kasulu wanapata shida kuwajibu Wananchi dhidi ya mgoholo unaoendelea katika poli la Kagerankanda Wananchi wanao kutwa Wakilima katika poli hilo wanapigwa na kunyanganywa vifaa vyao kwa madai kuwa hawaruhusiwi kulima katika poli hilo ilihali maeneo ya kulimia katika Wilaya hiyo ni Machache na Wananchi wengi wanategemea kulima Mahindi katika poli hilo.

  Kitowe alisema mpaka sasa Dawa zimeshafika katika Wilaya ya Kasulu iliwatu wa TFS waliopewa Dhamana ya kulinda msitu huo wamejipanga kumwagia Tindikari mahindi na Maharage yaliyo pandwa katika poli hilo hali inayoweza kupelekea Wilaya ya Kasulu na wilaya zingine za Mkoa wa Kigoma kukabiliwa na Njaa kwakuwa mazao yanayo limwa katika Msitu huo yanahudumia zaidi ya Wilaya nne za Mkoa wa Kigoma.

  Hata hivyo alisema endapo Mazao hayo yataunguzwa na Wananchi wakakosa haki yao na jasho lao likapotea jambo hili sio zuri mazao hayo yanapo vunwa Serikali inapata mapato lakini kila msimu wa mavuno halmashauri wanatoza kila gunia shilingi1000 na wanakusanya mapato Wananchi wengi wanasomesha watoto wao kupitia kilomo wanacho fanya katika poli hilo endapo jambo hilo likifanyika wananchi wengi wataumizwa na kitendo hicho.

  " nimuombe Muheshimiwa Rais yeye kama Mwenyekiti wetu wa Chama kilichopo madarakani atusaidie juu ya suala hili ilituweze kulitatua Wananchi wetu wanateseka sana juu ya Mgogoro huuu ,naikumbukwe Rais wetu aliwaahidi Wananchi katika Uwanja Wa umoja Wilayani Kasulu kuwa jambo la kwanza kulitatua itakuwa ni Mgogoro wa Msitu wa Kagerankanda uliodumu kwa kipindi cha Muda mrefu na Suala hili hata kwenye ilani yetu ya Chama lipo",alisema Kitowe.

  Nae Mbunge wa Kasulu Vijijini ,Vuma Holle alisema Suala hilo la Hifadhi ya poli la Kagerankanda amekwasha lipeleka Wizarani na Wizara inalitambua suala hilo linasubili sheria zikamilike na liweze kutatuliwa wananchi waweze kunufaika na maeneo yao.

  Alisema Wananchi wa Kasulu ni wengi sana na maeneo hayo hayawatoshi waongezewe mipaka Waweze kulima kwakuwa Wengi wao wanategemea kilimo jambo ambalo linaweza kuwa suruhisho kwa Suala hilo ni kuongeza mipaka ya Wakulima iliwaweze kulima.

  Aidha Holle alimuomba Rais kulitatua Suala hilo la Wananchi kuchomewa mazao yao suala linaloweza kuhatalisha hali za Wananchi Wa Wilaya ya Kasulu hali inayoweza kupelekea njaa katika Wilaya hiyo.

  0 0

  Na Rhoda Ezekiel Kigoma.

  MKUU wa Mkoa wa Kigoma , Brigedia Jenerali msaafu Emanuel Maganga amewataka Wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuacha tabia ya kudai fidia mara mbili katika maeneo yao yanayo chukuliwa kwaajili ya kufanyiwa uwekezaji wa viwanda na uchumi hali inayopelekea Mkoa huo kushindwa kuendelea kwasababu ya Baadhi ya watu wanaong'ang'ania maeneo kwa kudai walipwe fidia ya ziada.

  Rai hiyo aliitoa jana wakati akitoa salamu za Mwaka mpya kwa Wananchi wa Mkoa huo katika kanisa la Kiinjili la kiruthel Tanzania KKKT ushirika wa Kigoma alisema Mkoa wa kigoma kwa mwaka 2017 tumeandaa kubolesha Uchumi kwa kuanzisha viwanda vingi na kutenga maeneo kwaajili ya Shughuli za kiuchumi jambo ambalo litasaidia mkoa huu kufunguka kiuchumi.

  Maganga alisema kumekuwa na tabia ya Wananchi wengi wa Mkoa wa huu kudai fidia mara mbili unakuta eneo moja wanakuja watu zaidi ya wawili kudai fidia ya sehemu moja hali inayo pelekea Serikali kushindwa kufikia malengo yake kwakuwa fedha inayotengwa kwaajili ya suala la kuwekeza kwenye uchumi inaishia kuwalipa watu fidia tumeyaona hayo wakati wa kulipa fidia kwa eneo tunalo tarajia kujenga Bandari ya Nchi kavu.

  "Serikali ya Mkoa wa Kigoma kwa mwaka uliopita tumejitahidi sana kubolesha huduma za Kijami ikiwa ni pamoja na elimu ambayo imetuletea matokeo mazuri kwa mwaka uliopita Mkoa wa Kigoma umeshika nafasi ya kwanza kitaifa na umeongoza kwa asilimia 94% kwa mwaka huu kipaumbele chetu ni kuhakikisha tunakuza uchumi wa Mkoa wetu,"alisema Maganga.

  Alisema kuanzia sasa utaandaliwa utaratibu utakao saidia kujua ninani anastahili kulipwa fidia na kila eneo moja atalipwa Mtu mmoja watu wasitumie Fulsa ya uwekezaji wa Serikali kama njia ya kutajilika na kupatia mitaji tutajitahidi kufanya kazi hii kwa ufanisi ilikuhakikisha malengo tuliyo yaweka kwa mwaka huu yanakamilika.

  Aidha Maganga amewaomba Wananchi kufanya kazi kwa bidii na kuwaahidi huduma zote zitakazo tolewa na Serikali yake zitakuwa nzuri na zenye lengo la kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini iliwaweze kuinuka na kufikia uchumi wa kati kwa kubolesha miundombini mbalimbali ya kijamii itakayo fungua Fulsa za maendeleo ya Mkoa huo.

  Aliwaomba wafanya biashara kusafilisha bidhaa mbalimbali kupeleka nje ya Mkoa wa Kigoma kwa kutumia barabara zilizo jengwa vizuri kwa mwaka huu ilikuhakikisha Uchumi wa Mkoa wa Kigoma unakuwa kwa kasi na kwa kiwango cha juu.

  Nae Mchungaji wa Ushirika wa kanisa la Kiinjili la Kiruthali Mkoa wa Kigoma Emanuel Mtoi aliiomba serikali kuwahurumia Wanachi kwa kuwaboleshea huduma za kufanyia biashara na kuwawekea miundombinu mizuri ya kuwawezesha kufanya biashara bila kubuguziwa.

  Alisema Mwaka huu wananchi wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuweka malengo na mikakati itakayo wasaidia kujikwamua kiuchumi na kuacha kuilaumu serikali kwamba imebana hela na kushindwa kufanya kazi iliwapate fedha.

  0 0

  Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akikagua moja ya shamba la mahindi lililoharibiwa na tembo katika kijiji cha Kunzugu, wilaya ya Bunda Mkoani Mara jana  wakati wa ziara yake ya kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili. 
  Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kunzugu, wilaya ya Bunda, mkoani Mara jana alipotembelea moja ya shamba la mahindi lilioharibiwa na tembo wakati wa ziara yake ya kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili.


  NA HAMZA TEMBA - WMU
  .......................................................
  Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema italipa madeni yote ya miaka ya nyuma ya vifuta jasho na vifuta machozi ambayo inadaiwa na wananchi waliokubwa na vitendo vya uharibifu wa wanyamapori nchini kabla ya bunge lijalo la bajeti, madeni hayo ni yale ambayo yameshaifikia wizara hiyo na kuhakikiwa. 

  Akizungumza jana na uongozi wa wilaya ya Bunda wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku moja ya kufuatilia changamoto za uhifadhi wilayani humo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani amesema uamuzi huo wa Serikali utaondoa kilio cha muda mrefu cha wananchi ambao wamepata madhara mbalimbali ya wanyamapori ikiwemo vifo, majeruhi, kuliwa mazao na kuharibiwa mashamba yao. 

  "Serikali ya awamu ya tano imeshakamilisha takwimu za madai, yale yote tunayodaiwa huko nyuma, yaliyoifikia Wizara yakafanyiwa uhakiki na nimesema kwenye uhakiki huo ndani ya kipindi cha miaka kumi, kwa wilaya zaidi kidogo ya 80 ambazo ndizo zina changamoto hizi kwa kiwango kikuu, deni jumla ni shilingi 2,081,532,700 (bil. 2.9)", amesema. 

  Amesema wilaya ambazo zimeathirika zaidi na vitendo hivyo na ambazo madai yao ni makubwa zaidi ya Wilaya zingine ni Serengeti na Bunda ambazo ziko mkoani Mara na zinapakana na Hifadhi ya taifa ya Serengeti, Ziwa Victoria, Pori la Akiba Grumeti na Ikorongo. "Serengeti ndiyo inayoongooza kwa madai hayo, shilingi milioni 408,547,600 alafu Bunda shilingi milioni 265,969,750",. 

  Pamoja na Serikali kujiwekea utaratibu huo na wananchi wa kulipa vifuta jasho na vifuta machozi kwa waathirika, amesema ipo haja ya kutafuta njia endelevu ya kukabiliana na changamoto hizo na fedha ambayo ingetumika kulipia fidia hizo ikatumika kuwezesha mpango huo endelevu. Amesema mpango huo utawezekana kwa kuwashirikisha wananchi.

  "Mpango endelevu wa kukabiliana na changamoto hiyo ni ule wa ushiriki wa pamoja wa Serikali na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uharibifu dhidi ya wanyamapori", amesema. 

  Ili kufanikisha mpango huo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Bunda na Serengeti kuratibu ushiriki wa wananchi wao katika zoezi hilo kwa kuunda vikundi shirikishi katika kila kijiji, kubaini mahitaji yake ikiwemo vifaa na kuwasilisha taarifa hiyo wizarani kabla ya tarehe 15 januari mwaka huu, kwa ajili ya hatua zaidi za kufanikisha mpango huo. 

  Amesema ushirikiano huo pekee hautoshi kukabiliana na changamoto hizo kama wananchi nao hawataipunguzia mzigo serikali wa kupambana na vitendo vyao viovu dhidi ya uhifadhi, ili nguvu hiyo itumike katika kushirikiana nao kwenye ulinzi dhidi ya wanyama waharibifu. "Wananchi waache vitendo viovu dhidi ya uhifadhi, ujangili, kuua wanyamapori",. 

  Ameeleza kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa changamoto hizo ni matokeo ya tabia za wananchi kusogelea maeneo ya hifadhi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, jambo ambalo lina athari kubwa katika uhifadhi na usalama wa wananchi wenyewe, hivyo ni lazima liepukwe.

  "Njia ambayo tembo alikua akipita miaka 20, 30, 40 ndo anapita kila siku, sisi tumeenda kujenga, tumeenda kulima mashamba, sasa tembo wao na wenyewe wana ownership (umiliki), ile njia wao wanaona ni ya kwao tu, kwahiyo akikutana na wewe anafanya hayo anayoyafanya, hata kwenda kukaa kufanya shughuli za kibinaadamu ikiwemo kujenga na kulima jirani kabisa na kwenye mpaka ya hifadhi na yenyewe ni tatizo". 

  Naibu Waziri Makani amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mara jana ambapo alitembelea vijiji kadhaa wilayani Bunda na Serengeti na kushudia athari mbalimbali za uharibifu wa wanyamapori pamoja na kupokea malalamiko mbalimbali ya uharibifu huo kutoka kwa wananchi. Alishuhudia mashamba kadhaa ya mahindi yaliyokuwa karibu na maeneo ya hifadhi yakiwa yameharibiwa na tembo.

  0 0


  0 0


   Nabii mkuu mheshimiwa Dr Geordavie akiombea  bajeti mbalimbali  za waumini walizoziletwa kwa ajili ya kutolewa neno la unabii hiii leo


  Na Woinde Shizza,Arusha.  Watanzania nchini wametakiwa kusaidia Jamii ya watu wasiojiweza ikiwemo walemavu,watoto yatima pamoja na wazee ili waweze kupata mahitaji yao na kuondokana na umasikini uliokithiri.  Hayo yameelezwa na Baadhi ya Wananchi waishio katika kata ya Kisongo mkoani Arusha ambapo walisema kuwa jamii ya wahitaji imekua ikiishi katika mazingira magumu hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha kuwa anawasaidia jamii hiyo.

  "katika jamii kuna watu wengi wakiwemo watoto wanatoto na watu wasio jiweza ambao wanakaa katika mazingira magumu mno  hivyo ni wajibu wetu sisi kuwasiaidia wale ambao awajiwezi ,mtu ukiwa na uwezao kidogo unatakiwa ujijengee tabia ya kuwasiaida hawa wasio jiweza"alisema Sekela Tondolo  Kwa upande wake Mkazi mwingine wa kata ya  Kisongo Wiliam James Alisema kuwa  jamii ya wasiojiweza imekua ikisahaulika mara kwa mara hivyo ni jukumu la kila Mwananchi kuhakikisha kuwa anafanya kitu kwa ajili ya jamii yake kitakacholeta mchango ambao ni chanya na kuwawezesha kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo kimaisha.  Kwa upande wake Mheshimiwa Nabii Mkuu Dr. Geor  Davie  wa Huduma ya Ngurumo ya Upako  katika ibada ya makusanyo ya vitu na fedha kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji alisema kuwa taasisi za dini hazina budi kujikita katika kuwasaidia wahitaji na wasiojiweza ili kuwa na taifa imara na endelevu .

  "ni wajibu wa taasisi za kidini  ,makampuni mbalimbali , hata watu binafsi ambao wanauwezo kuweza kusaidia watu hawa wenye mahitaji na walae wasio jiweza ili nao wajisikie vyema na kuona nao  ni sehemu ya watu kama wengine "alisema  Geor  Davie  Huduma hiyo inautaratibu endelevu wa kila mwaka wa kupeleka mahitaji kwa wato wasiojiweza pamoja na kuwawezesha kiuchumi kaya zilizoathiriwa na umasikini kwa kiasi kikubwa.


  0 0

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani ambaye amelazwa katika hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es salaam akitibiwa Januari 2, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

  WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtembelea na kumpa pole Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mhe. Steven Ngonyani (Profesa Majimarefu) aliyelazwa katika Hospitali ya Kairuki akipatiwa matibabu.
  Akiwa hospitalini hapo leo (Jumatatu, Januari 2, 2017), Waziri Mkuu amesema amefurahi baada ya kumkuta Mbunge huyo anaendelea vizuri na kwamba afya yake inaridhisha.

  Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumtakia afya njema Mhe. Ngonyani. Amesema anaamini hivi karibuni atapona na kuruhusiwa kutoka hospitali.
  Kwa upande wake Mbunge huyo ambaye amelazwa katika hospitali ya Kairuki iliyoko Mikocheni jijini  Dar es Salaam, amemshukuru Waziri Mkuu kwa kwenda kumjulia hali.

  Pia amesema anaendelea vizuri na anatarajia kwenda nchini India kwa matibabu zaidi mara taratibu zitakapokamilika.

   IMETOLEWA NA:
  OFISI YA WAZIRI MKUU,
  2 MTAA WA MAGOGONI,
  S.  L. P. 3021,
  JUMATATU, JANUARI 2, 2017.

  0 0

  Na. Lilian Lundo – MAELEZO

  Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imedhamini mashindano ya Soka la ufukweni kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Jijini Dar es Salaam yanayotarajiwa kufanyika katika fukwe za Coco Januari 07 mwaka huu.

  Afisa Mkuu wa Mauzo kutoka Kampuni hiyo Peter Ngota ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya udhamini huo.

  Aliendelea kwa kusema kuwa, mashindano hayo yanawalenga wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Jijini Dar es Salaam ambao ni wadau wakubwa wa Kampuni ya TTCL kupitia huduma ambazo wanazitoa kama vile vifurushi vya intanenti, dakika pamoja na ujumbe mfupi.

  “Tumeamua kudhamini mashindano hayo kwa wanafunzi hao kutokana na umuhimu wa michezo kwao katika kuwajengea amani, furaha na afya njema ambavyo vitawawezesha kufanya vizuri katika masomo yao na hata kuwa wabunifu katika maeneo wanayosomea na kupelekea nchi kufikia uchumi wa kati,” alifafanua Ngota.

  Kwa upande wake kocha Mkuu wa mashindano hayo John Mwansasu ameishukuru Kampuni ya TTCL kwa kudhamini mashindano hayo ambayo bado hayajapata umaarufu mkubwa hapa nchini.

  Aidha amesema kuwa, ili kuwapa uzoefu washiriki wa mashindano hayo, kutakuwepo na wachezaji ambao walichezea timu za Simba na Yanga ambao pia watacheza kutokana na timu ambazo walikuwa wakichezea.

  Vilevile Mwansasu amesema kuwa, wataendelea kushirikiana na Kampuni ya TTCL ili kusambaza mchezo huo katika mikoa yote ya Tanzania.

  Vyuo vilivyothibitisha ushiriki wa mashindano hayo mpaka sasa ni Chuo cha Biashara (CBE), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu Huria (OUT), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT). Mashindano hayo hayatakuuwa na kiingilio na yataanza saa 3:00 asubuhi.

  0 0  0 0

  MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa kupinga sheria ya mtandao iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015 ili kulinda maslahi ya Taifa ya kupambana na kutoa mwelekeo wa kukabiliana na makosa ya mtandao.

  Hukumu hiyo ya kihistoria ilitolewa na jopo la majaji watatu, Prof. John Ruhangisa, Winfrida Korosso na Lugano Mwandambo mara baada kuona hoja zilizowalishwa na wakili wa kujitegemea Jebra Kambole kuwa hazina msingi.

  Hata hivyo, mahakama hiyo imetoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya marekebisho kwenye kifungu kimoja kati ya 18 vya sheria hiyo vilivyokuwa vikilalamikiwa kwa vile kifungu hicho kinakiuka haki ya msingi ya mwananchi ya kusikilizwa.

  Pamoja na kutoa maelekezo hayo, mahakama imeona vifungu vingine ndani ya sheria hiyo havikuwa na mapungufu yoyote ya kikatiba kama ilivyokuwa inadaiwa na mwombaji (Kambole).

  Katika malalamiko yake, Kambole alidai kuwa Sheria ya mtandao ilikuwa na baadhi ya maneno ambayo hayakutafasiriwa ambavyo kwa namna moja au nyingine vingeweza kuchambuliwa vibaya na vyombo vya usalama na hivyo kumwonea mwananchi.

  Hata hiyo, jopo la majaji hao waliona hoja hizo hazina mashiko mara baada ya kupitia kwa kina vifungu vya Sheria husika na kuona kuwa vifungu hivyo lalamikiwa vinaainisha kosa ambalo linaweza kutendeka na kutoa adhabu inayotakiwa.

  Majaji hao wamebainisha kuwa vifungu namba 4, 5, 6, 7, 8, 9, 14, 19, 21 na 22 vya sheria ya mtandao vilivyolalamikiwa vinaenda sambamba na Ibara ya 17 (2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo haviwezi kwenda kinyume na katiba.

  Kwa mujibu wa jopo hilo, mwananchi anayonafasi ya kupinga maamuzi yanayotolewa na kiongozi kwa kupeleka maombi ya mapitio (judicial review) mahakama kuu kama itabainika kuwa alienda kinyume na madaraka yake aliyopewa kisheria.

  Mara baada ya kufikia uamuzi kuwa vifungu hivyo vya sheria ya mtandao havikinzani na Ibara ya 17 (2), 20 (5) na 30 (2) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, majaji hao walikataa wito wa mlalamikaji wa kuviona vifungu hivyo vinakiuka katiba.

  Kambole katika maombi yake alilalamikia pia vifungu namba 38 na 50 vya sheria ya mtandao kwamba vinakiuka Ibara ya 13 ya Katiba juu ya mwananchi kuwa na haki ya kusikilizwa.

  Mlalamikaji huyo alidai kuwa kifungu namba 38 kinatoa uhuru kwa mamlaka kupeleka maombi mahakamani ambayo yanaweza kusikilizwa kupitia upande mmoja bila upande wa pili katika maombi hayo kuhusishwa.

  Hata hivyo, majaji hao walibainisha kuwa kifungu hicho kinahusiana na maswala ya kufanya upekuzi, kukamata, kukusanya na kuweka wazi takwimu kwa lengo la upelelezi. Katika mazingira hayo, majaji waliona kuwa malalamiko yaliyotolewa hayakuwa na msingi wowote kwa vile maswala ya upelelezi hayatoi ukomo katika kutatua haki ya mwananchi.

  0 0

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumatatu  Januari mbili, 2017 amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Kagera kwa kuwatembelea baadhi ya wananchi walioathiriwa na tetemeko la ardhi pamoja na kukagua baadhi ya miundo mbinu iliyoathiriwa na tetemeko hilo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari ya Ihungo  Omumwani iliyobomolewa na tetemeko la ardhi la Septemba 10,2016.
  Mara baada ya ukaguzi huo Rais Dkt Magufuli akazungumza na wananchi wa Mkoa huo wa Kagera katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ihungo na kuagiza kuvunjwa kwa kamati ya maafa ya Mkoa huo iliyokuwa ikiratibu utoaji wa misaaada na kufanya tathmini ya athari ya tetemeko hilo.
  ”Kila kitu huwa kina mwanzo na mwisho wake ukiwa na harusi huwa kuna kamati ya harusi,ukishamaliza kufunga ndoa kamati ya harusi huwa inavunjwa,na ukiwa kwenye msiba huwa kuna kamati ya msiba na msiba  mkishazika kamati ya mazishi huvunjwa,kamati ya maafa ya Kagera huu ni mwezi wa tano na inawezekana hata kwenye kamati huwa wanalipana posho,sasa nataka hii kamati nayo iishe,yalishapita yamepita”
  Aidha Dkt Magufuli amewataka wote walioahidi kuchangia katika kamati ya tetemeko la ardhi ya mkoa wa Kagera ambao bado hawajatekeleza ahadi zao ambazo ni jumla ya shilingi bilioni nne nukta tano wakamilishe ahadi hizo ili ziweze kumalizia miundombinu ya Serikali iliyoathiriwa na tetemeko hilo.
  Ameongeza kuwa wale wote wanaoendelea kuguswa kusaidia wapeleke michango yao moja kwa moja kwa wananchi badala ya kuipeleka serikalini kwa kuwa hakuna mchango mwingine utakaopokelewa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
  Pia Rais Dkt Magufuli ameagiza shule ya Sekondari ya Omumwani iliyokuwa inamilikiwa na Jumuia ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM imilikiwe na Serikali kutaka wanafunzi wote wanaosoma katika shule hiyo kutolipa ada kama zilivyo shule nyingine za serikali.
  Dkt Magufuli ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kupunguza utitiri wa kodi katika zao la kahawa ili bei ya zao hilo ipande na kuwanufaisha wakulima
  Balozi wa Uingereza hapa Nchini Bi Sarah Cooke ambaye nchi yake imechangia kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Ihungo, amempongeza Rais Dkt Magufuli na serikali yake kwa jitihada za kupambana na rushwa suala ambalo nchi yake ya Uingereza inalipa kipaumbele sambamba na kutoa elimu bila malipo jambo linalowawezesha watoto wengi wa kitanzania kupata elimu bure
  Jaffar Haniu
  Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
  Kagera.
  02 Januari, 2017

  0 0

  Na Daudi Manongi – MAELEZO.

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wakuu wa Mikoa,Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuondoa utitiri wa kodi uliopo kwenye Mazao ili wakulima waweze kunufaika kutokana na kujiongezea kipato.

  Agizo hilo alimetolewa leo wakati akihutubia wakazi wa Wilaya ya Bukoba na watanzania kwa ujumla akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kagera.

  “Nawaagiza Wakuu wa Mikoa,Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kupitia upya Kodi zilizopo katika bidhaa mbalimbali kama Kahawa na Pamba, hakikisheni mnaondoa utitiri huu wa Kodi ili wafanyabiashara hawa wafaidike na mazao yao,” Alisema Rais Magufuli.

  Aidha Rais Magufuli amewaahidi watanzania kuwa atahakikisha anafanya kazi usiku na mchana bila kujali itikadi, dini na makabila ili kuhakikisha nchi inasonga mbele katika nyanja zote za kimaendeleo.

  Akizungumzia maendeleo ya michango mbalimbali kwa ajili ya wathirika wa tetemeko la Ardhi mkoani Kagera Rais Magufuli amesema kuwa mpaka sasa simenti iliyochangwa ni zaidi ya tani 30,600 na mabati zaidi ya elfu 31,000 ambapo wananchi wameshaanza kupewa na kujengea.

  Amewahimiza wananchi walioathirika na tetemeko la Ardhi kutotegemea Serikali kuwafanyia kila kitu na badala yake waanze kujenga na watumie msimu huu wa mvua kulima ili kujipatia chakula.

  Pia Rais Magufuli amewashukuru na kuwapongeza wahisani waliochangia Maafa ya Kagera na kuwataka kuendelea na moyo huo katika kulijenga Taifa letu.

  0 0

  Aonya wanaokata miti ovyo, asisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji

  WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya wakazi wa Ruangwa wanaokata miti kwenye misitu waache kufanya hivyo mara moja ili kuokoa ardhi chepechepe waliyokuwa nayo.

  Amesema ukataji miti huo unafanywa zaidi na watu wanaoanzisha mashamba ya ufuta na wapo walioamua kulima karibu na vyanzo vya maji hali iliyosababisha maji yakauke kwenye maeneo mengi.

  “Zamani kuna maeneo ulikuwa haupiti hadi ukunje suruali, na kama una gari napo pia ilikuwa ni taabu kupita kwenye maeneo hayo. Lakini sasa hivi, hakuna tena maeneo hayo ndiyo maana kila unakopita unakuta akinamama wanatembea mwendo mrefu na ndoo huku vijana wakibeba madumu kwenye baiskeli nao wakitafuta maji,” alisema Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa.

  Ametoa onyo hilo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wakazi wa vijiji mbalimbali vya  wilaya hiyo ambao walifika Ruangwa mjini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM kusikiliza taarifa ya mambo aliyoyafanya jimboni humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

  “Kilimo cha ufuta kimekuwa balaa, sasa hivi hakuna maji sababu ya ukataji miti ovyo. Mfano mzuri ni mto Mbwemkuru ambao ulikuwa ukitiririsha maji mwaka mzima, angalia sasa hivi, umegeuka kuwa mto wa msimu na chanzo ni ukataji wa miti,” alisisitiza.

  “Tusipobadilika na kuacha hiyo tabia tutamlaumu mbunge na Serikali kuwa hawaleti maji wakati sisi wenyewe tumechangia hali hiyo kwa kuharibu vyanzo vya maji,” alionya na kuongeza kuwa amelazimika kutafuta mashine ya kuchimba maji ili kupunguza tatizo la maji.

  Alisema mapema mwaka huu, wataalamu wataanza kufanya utafiti ili kubaini maji yako umbali gani kwenda ardhini kabla ya kuanza kuchimba visima hivyo. “Ikibidi tutaaza na visima vifupi na vya kati ili maji yapatikane haraka,” alisema.

  Akielezea mipango ya mwaka huu kwenye sekta ya afya, Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi wa jimbo hilo kwamba anatamani kuona kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kupunguza umbali wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa vijijini.

  “Kila nilikopita vijijini nimewahamasisha wananchi waanze kufyatua mafotali ili ujenzi wa boma ya zahanati uanze. Na mimi nimeahidi kuchangia mabati kwa kila zahanati, na kuna baadhi ya maeneo nimechangia hata mabati ya nyumba ya mganga na muuguzi,” alisema.

  Alisema mwaka uliopita, alifanikiwa kukamilisha ujenzi wa wodi ya akinababa, ya akinamama na kukarabati wodi ya magonjwa mchanganyiko katika hospitali ya wilaya ambapo fedha taslimu milioni 100 zilitumika. Pia aliwezesha kufunga umeme wa jua kwenye zahanati zote zinazotoa huduma za afya ndani ya jimbo na kazi hiyo itaendelea kwa awamu ya pili.

  “Pia niliweza kulipia kaya 10 zisizokuwa na uwezo kwa kila kijiji ili zijiunge na mfuko wa afya ya Jamii (CHF) kwa gharama za shilingi milioni 9. Jumla ya vijiji 92 vimefikiwa. Ninawasihi wana-Ruangwa kila mmoja ajiunge na mfuko huu ili muweze kupatiwa huduma za afya bila matatizo,” aliongeza.

  Akielezea kuhusu sekta ya elimu, Waziri Mkuu alisema ameweza kufadhili ujenzi wa matundu ya vyoo 70 Katika shule za msingi saba ambapo kila shule imejengewa matundu 10 (manne wavulana, manne wasichana na mawili kwa walimu) ambapo jumla ya sh. milioni 63 zimetumika. Alisema kazi hiyo itaendelea awamu ya pili.

  “Zaidi ya hayo, nimefanikisha ufungaji wa umeme jua kwenye shule za sekondari nne za Chunyu, Makanjiro, Narungombe na Nambilanje. Katika awamu ya kwanza tumekamilisha kuweka umemejua kwenye sekondari za tarafa ya Mandawa, na tarafa ya Ruangwa imefikiwa nusu tu. Katika awamu ya pili, tutamalizia tarafa ya Ruangwa na kukamilisha tarafa nzima ya Mnacho,” alisema.


  IMETOLEWA NA
  OFISI YA WAZIRI MKUU
  JUMATATU, JANUARI 2, 2017.

  0 0

  Mwenye fulana ya damu ya mzee ni Pius Malindisa ambaye ni mdogo wake marehemu.Nyumbani kwa kwa marehemu ATANAS PATRICK watu wakiwa wamejitokeza kwa ajili ya kwenda kumstili.

  Na Amon Mtega

  JESHI la polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Patrick Malindisa [29 makazi wa mtaa wa Namanyigu kata ya Mshangano Manispaa ya Songea mkoani humo kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi Atanasi Malindisa [70] kwa kumpiga na kitu chenye ncha butu kichwani na kidevuni upande wa kushoto kisha kufanya jaribio la kuchimba shimo kwenye nyumba hiyo kwa malengo ya kumzikia baba huyo.

  Akizungumza na Ruvuma TV katika eneo la tukio mmoja wa wanafamilia ambaye ni mdogo wa marehemu Piusi Malindisa alisema kuwa wao walipata taarifa ya kifo cha ndugu yao Januari Mosi mwaka huu majira ya 1.30 kutoka kwa mtoto wa marehemu Patrck Malindisa .

  Piusi alisema kuwa mtoto huyo ambaye alikuwa akiishi kwenye nyumba hiyo na marehemu huyo alitoa taarifa kwa wanandugu kuwa baba yake amefariki kwa homa ya tumbo na ndugu walipofika kabla ya kuingia chumbani alikokuwa akilala marehemu waliamua kuuita uongozi wa mtaa ambao uliingia na kubaini kuwa Atanasi Malindisa ameuwawa kwa kupigwa na kitu kichwani na kidevuni.

  Alisema kuwa baada ya kubaini hilo walitoa taarifa polisi kisha mwili huo ulichukuliwa na kwenda kuuhifadhi Hospital ya mkoa Ruvuma [HOMSO] kwa uchunguzi huku jeshi la polisi likimshikilia mtoto wa marehemu kwa mahojiano zaidi.

  Alifafanu kuwa polisi wakiwa bado kwenye nyumba hiyo walibaini kuwa kwenye moja ya chumba ambacho hakijaezekwa kulichimbwa shimo linaloendana na vipimo vya marehemu ambalo lilihisiwa kuwa alitaka amfukie humo ili watu wasijue kwa kuwa kwenye nyumba hiyo walikuwa wakiishi wawili.

  “Uchimbaji wa shimo hilo lenye mithiri ya kaburi lilimshinda kisha akamua kulifukia na kuchukua hatua ya kuja kutoa taarifa kwetu wanandugu kuwa baba yake amefariki kwa homa ya tumbo ambayo inadaiwa alikuwa akilia nalo kumbe sivyo bali kapigwa na kitu kichwani”alisema Ndugu wa marehemu.

  Kwa upande wake jirani wa nyumba hiyo ambaye hakutaka kulitaja jina lake alisema kuwa maisha ya marehemu na mtoto wake walikuwa wakipigana mara kwa mara hasa kwa kutumia silaha na majirani walikuwa hawapo karibu nao kutokana na tabia hizo.

  Vituko vya tawala kwenye makaburi ya Namanyigu wakati wa uchimbaji wa kaburi la kumzikia marehemu Atanasi Malindisa ambako mtandao huu umeshuhudiwa vijana walitaka kugomea kuchimba kaburi hilo kwa madai kuwa familia hiyo ilikuwa haijihusishi kwenye matatizo ya majirani.

  Baadhi ya wazee waliwasii vijana hao kwa kuwaomba wasilipe ubaya kwa ubaya cha msingi wafanikishe kumuhifadhi marehemu kwa kuwa marehemu hayupo duniani hivyo ni vema wakasamehe na kumuachia Mungu.

  Katika usafirisaji wa mwili huo kutoka katika Hospital ulikohifadhiwa baada ya magari ya maeneo hayo kutokuonyesha nia ya kutoa msaada gari la Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas Gama ambalo alilitoa kwa wananchi kwaajili ya matatizo mbalimbali la okoa jahazi kwa kuubeba mwili wa marehemu huyo.

  Naye kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Zuberi Mwombeji amethibitisha kutokea kwa tukio hilo pamoja na kumshikilia mtuhumiwa Patrick Malindisa mtoto wa marehemu na kuwa jeshi hilo linaendelea na upelelezi likiwemo shimo lililokutwa.


  0 0

   Mbunge wa Musoma Vijijini na muandaaji wa Mashindano ya mitumbwi Musoma vijijini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza baada ya mashindano.
   Washindani wakiendelea na mashindano ndani ya ziwa Victoria katika kata ya Etaro, Musoma Vijijini
   Wananchi wa Musoma Vijijini wakishangilia wakati wa mashindano ya Mitumbwi
   Timu ya International iliyoshika nafasi ya mwisho ikiwasili
   Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Vijijini na Diwani wa Kata ya Mugango, Charles Magoma (kushoto) akikabidhi zawadi kwa washindi wa kwanza.
  Vijana kutoka Kata ya Suguti ambao walishika nafasi ya Tatu wakishangilia mara baada ya mtumbwi wao kuwasili


  Mashindano ya Mitumbwi Musoma Vijiji yaliyoshirikisha Kata 12 yamemalizika kwa Kata ya Etaro kuibuka na ushindi na hivyo kujinyakulia fedha tasilimu milioni moja pamoja na kombe.

  Mashindano hayo yaliandaliwa hivi karibuni na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo kwa ajili ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 ambapo washindi wa pili ambao ni Kata ya Nyakatende walijinyakulia shilingi 750,000 na washindi wa tatu ambao ni Kata ya Suguti kujinyakulia shilingi 500,000 na huku wanaofuatia walipata shilingi 20,000 kwa kila Kata.

  Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Vijijini na Diwani wa Kata ya Mugango, Charles Magoma, alimpongeza Profesa Muhongo kwa kuanzisha mashindano ya namna hiyo jimboni humo kwani yamekutanisha wananchi wa Musoma Vijijini kutoka pande mbalimbali za jimbo hilo.

  Aliongeza kwamba mashindano hayo yameleta mwamko mkubwa miongoni mwa vijana hasa ikizingatiwa kuwa hakuna mashindano ambayo huwakutanisha vijana kwa wingi kama ilivyokuwa kwa mashindano hayo ya mtumbwi.

  Kwa upande wake, mbunge wa jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo alisema aliamua kuandaa mashindano hayo na mengine ya ngoma za asili na kuimba kwaya ili kuwakutanisha wanamusoma vijijini kwa maendeleo ya afya zao na jimbo kwa ujumla.

  Alisema njia mojawapo ya kuwa na afya bora ni kushiriki michezo mbalimbali na hivyo aliahidi mashindano mengine ya mieleka ambayo yatafanyikia kwenye Kata ya Mugango mapema mwezi Aprili.

  Aliwataka wananchi hususan vijana kujitokeza kwa wingi na kwamba washindi watapewa zawadi ambayo alisema ataitangaza siku nyingine.
  Aidha, alisema kila Kata iandae washiriki wawili kwa ajili ya kushiriki mieleka na wananchi wajiandae kushuhudia mashindano hayo ya kihistoria kuwahi kutokea Musoma Vijijini.

  Mashindano hayo ya mitumbwi jimboni humo yalishirikisha jumla ya Kata tisa huku kila mtumbwi ukiwa na washiriki kati ya watano hadi saba na vilevile timu moja ya kimataifa ya rafiki zake na mbunge huyo kutoka Ujerumani ilishiriki na kushika nafasi ya mwisho.


  0 0

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaolon Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.Mazungumzo hayo yalikuwa na lengo la kuushukuru Ubalozi wa Ubalozi huo kwa kufanikisha uratibu wa Ziara ya Kiserikali ya Balozi Seif aliyoifanya hivi karibuni Nchini China.

  Picha na – OMPR – ZNZ.
   
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Ubalozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China uliopo Zanzibar kwa maandalizi mazuri iliyofanya kuratibu ratiba ya ziara yake ya Siku Tano aliyoifanya hivi karibuni Nchini China.

  Alisema ziara hiyo ya Kiserikali ilimuwezesha na kumpa fursa ya kukutana na Uongozi wa Kampuni na Taasisi mbali mbali za China zilizoonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi vyao Visiwani Zanzibar.

  Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Bwana Xie Xiaolon akimshukuru kwa kukamilisha ziara hiyo kwa mafanikio makubwa.

  Alisema Mikutano ya pamoja kati ya Ujumbe wa Zanzibar na Uongozi na Makampuni mbali mbali waliyokutana nayo yalikuwa na muelekeo mwema wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

  “ Ratiba yote iliyopangwa ndani ya ziara hiyo imetekelezwa kwa asilimia kubwa na kuonyesha matumaini mapya ya ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla”. Alisema Balozi Seif.

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar kwamba Makampuni ya Umeme ya TBEA, Uvuvi ya Hongdong, ile inayotoa huduma za Kijamii ya Avic pamoja na Kampuni ya MCC – Oversease tayari wataalamu wake wameshaangalia mazingira ya Zanzibar na kujiandaa namna ya kuanzisha miradi yao Zanzibar.

  Naye Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Xiaolon alisema Zanzibar na China daima zitaendelea kushirikiana katika njia ya uanzishwaji wa miradi ya pamoja itakayosaidia kuleta ustawi wa wananchi wa sehemu hizo mbili.

  Bwana Xie alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuona miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kupitia msaada au udhamini wa Serikali ya China itatekelezwa na kukamilika kama ilivyokusidiwa.

  Othman Khamis Ame
  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
   

older | 1 | .... | 1087 | 1088 | (Page 1089) | 1090 | 1091 | .... | 1897 | newer